×

Wajue Wanawake 5 Wanaoutikisa Ulimwengu wa Sayansi

1. Profesa Jocelyn Bell Burnell wa Ireland Kaskazini.

MWANAMKE huyu ni maarufu kwa uvumbuzi wa kwanza wa kidude kidogo cha amawasiliano ya kupitia angani kinachofahamika kama ‘pulsar’ kinachotuma mawimbi ya sauti ya redio zaidi ya miaka 50 iliyopita. Zaidi ya hapo,  Prof Dame Jocelyn Bell Burnell pia amekuwa mtetezi wa muda mrefu wa wanawake katika sayansi.

Akiwa mwanafunzi shuleni Ireland Kaskazini miaka ya 1950, kama wasichana wengine,  hakuruhusiwa kusoma masomo ya sayansi hadi wazazi wake na watu wengine walipopinga jambo hilo.

“Wavulana walipelekwa katika maabara ya sayansi na wasichana walikuwa wanapelekwa katika chumba cha sayansi-kimu kwa sababu kila mtu alifahamu kuwa wasichana walikuwa wanajiandaa kuolewa kwa hiyo walihitaji kujifunza jinsi ya kutandika vitanda,” anakumbushia.

Akiwa profesa wa masomo ya fizikia ya anga katika Chuo Kikuu cha Oxford, alikuwa ni mmoja wa wanawake wanasayansi ambao juhudi zao ziliwezesha kutolewa kwa tuzo za kutambua mchango wa wanawake wenye taaluma  hiyo.

“Mgawanyo wa kijinsia katika sayansi ni wa kitamaduni zaidi kuliko uwezo wa kiakili wa mwanamke na baadhi ya nchi zinafanya vyema kuliko nyingine.

“Katika fizikia ya  vyombo vya anga, nchi za kusini mwa bara la Ulaya kama Ufaransa, na Italia zimefanya vyema zaidi kuliko mataifa ya kaskazini mwa bara la Ulaya kama vile Ujerumani na Uholanzi.

“Katika nchi zote, idadi ya wanawake wanaojiunga na fani hiyo ya sayansi inaongezeka lakini hali imesalia kuwa kama ilivyo, jambo ambalo linafurahisha.  Mafanikio ni ya taratibu lakini  mambo yanabadilika polepole,” anasema profesa huyo.

 2. Kiongozi wa utafiti : Dkt Nicola Beer (Ujerumani)

Mapenzi ya Dkt. Nicola Beer katika masuala ya  sayansi yalianza wakati alipokuwa na umri mdogo.  Moja ya kumbukumbu zake ni kumtazama mwalimu wake akijaribu kuelezea dhana ya mawimbi ya sauti kwa kutumia kipande cha karatasi kilichojazwa mchele na kipaza sauti katika shule yao ya msingi.

Akiwa ndiye mtu wa kwanza wa familia kusoma masomo ya chuo kikuu, shahada yake ya kemia ya baiolojia katika Chuo Kikuu cha Bristol, ilimuwezesha kupata shahada ya uzamivu(PhD) katika chuo Kikuu cha Oxford  na kupata udhamini wa kimasomo nchini Marekani katika chuo cha MIT na Harvard kabla ya kuongoza timu ya watafiti.

Akiwa mkuu wa Idara ya Uvumbuzi wa Kibaiolojia na Kifamasia katika kituo cha Novo Nordisk katika Chuo Kikuu cha Oxford, Beer ni mkuu wa idara na sayansi.

“Ni suala la kupanga mkakati wa muongozo, kuwasaidia watu kuboresha mawazo yao, kuyatekeleza na pia kuwaunga mkono katika kazi zao ,” anasema na kuongeza kwamba anaamini kuwa kwa wanawake wachache  walio katika nafasi za uongozi,  wana wajibu wa kuungana mkono, kama washauri, kwa kueneza ujuzi na kufungua milango husika.

“Hicho ndicho kitu ninachofikiri tunapaswa kuwa tunakifanya wanawake wote. Tuna wajibu wa kutengeneza njia ya jinsi mambo yatakavyokuwa kuliko kulinda tu vyeo vyetu.  Ni muhimu tufanye hilo kwa ukarimu ,” anasema.

3 Mvumbuzi : Gladys Ngetich (Kenya)

Wakati Gladys Ngetich alipoambiwa kwenye mkutano kuwa “huonekani kama mhandisi”,  alikwenda nyumbani akijiuliza mhandisi anapaswa kuwa na sura gani.

Kama mwanafunzi wa utafiti akisomea uhandisi mitambo,  alikuwa amezowea kupambana na unyanyapaa. Wakati akisomea shahada ya uhandisi mitambo nchini Kenya,  alikuwa ni mwanafunzi pekee wa kike kati ya wanafunzi 80.

“Wengi miongoni mwa wanafunzi wa kiume walidhani sitaweza,” anasema  lakini alifaulu kwa alama za juu katika shahada yake. Hivi karibuni alimaliza masomo yake ya shahada ya uzamivu (PhD) katika uhandisi wa utengenezaji wa ndege na vyombo vya anga za mbali katika Chuo Kikuu cha Oxford.  Alishinda tuzo ya mwaka 2019 ya sayansi  ya Schmidth Science Fellowship kwa kuchunguza teknolojia za sayansi ya anga zinazosaidia maendeleo ya kudumu.

Akiiga mfano wa wanawake kama Profesa Bell Burnell, anataka kuwa mfano kwa vizazi vipya vya wahandisi.

“Ninatumai kutakuwa na orodha ya wanawake watakaokuja baada yangu,  na ni matumaini yangu kuwa hawatahitajika kujithibitisha utaalam wao kupita kiasi,”anasema.

4 Dkt Megan Wheeler (Marekani)

Ni vipi binadamu anatatua changamoto kubwa zinazoikabili dunia? Sayansi ina majibu, lakini kama tatizo hilo litaangaliwa kwa taswira tofauti. Hayo ndio maoni ya Dkt Megan Wheeler, ambaye kama Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa mpango wa HS Schidt Sience Fellowship,  ana mpango wa kuwapatia mafunzo wanasayansi wa kizazi kipya.

Dkt Wheeler ana shahada mbili za uzamivu katika sayansi ya ubongo katika Chuo Kikuu cha Oxford na saikolojia ya kliniki aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Marekani. kwa sasa anaongoza mpango unaolenga kuwanoa wanasayansi katika kukabilianana changamoto za dunia.

“Ninadhani kuwa ni muhimu kwamba tuwe na wanasayansi ambao si wenye uzoefu wa kina tu bali wawe pia na uwezo wa kuvuka mipaka yote hiyo ,” anafafanua.  na kusisitiza kwamba  kwa mwanasayansi leo inamaanisha kuwa na uwezo wa kutoka nje ya maabara na kuwasiliana na watu juu ya umuhimu wa kazi unayoifanya.

5. Elina Aino Johanna Pörsti (Finland)

Akiwa ni binti wa mwalimu wa fizikia na daktari, Elina Aino Johanna Pörsti alikulia nchini Finland katika familia iliyokuwa na msimamo wa  kupenda sayansi. Radi ilipopiga, baba yake alikuwa akiwaelezea fizikia nyuma ya radi inavyofanya kazi, huku mama yao akiwaelezea kuhusu mwili  mzima wa binadamu unavyofanya kazi.   Naye akiwa mtoto alionyesha moyo wa ujasiliamali, wakati alipofungua duka lake la dawa kwneye eneo la mwambao.

Shuleni alisomea masomo ya baiolojia kuhusu jeni, mambo ambayo yalimtayarisha kwa ajili ya kazi yake ya baadaye.

“Ni jambo la kufurahisha kwamba ungeweza kuondoa vinasaba (DNA) na kufanya kazi katika maabara na nilifikiri ilikuwa ni jambo  zuri sana na kitu ambacho ningekifanya.

“Kwangu mimi binafsi ninavutiwa na sayansi kwa sababu ninapenda kuelewa mambo mengi na huwa kuna mengi,” anasema.

Mwanamke huyo alisomea sayans katika Chuo Kikuu cha Helsinki na akapata shahada ya uzamili wa biashara kutoka Copenhagen. Kwa sasa ni mwanasayansi katika taasisi ya utafiti wa kisayansi ya Novo Nordisk ya Oxford akishughulikia uvumbuzi wa vifaa vya utambuzi wa magonjwa.

 

Chanzo BBC Swahili