×

Moto Wateketeza Ghala la Kiwanda, RPC Anena Mazito

MOTO mkubwa ambao chanzo chake hakijajulikana, umezuka na kuteketeza moja kati ya maghala matatu ya kuhifadhia pamba katika kiwanda cha Sunflag kilichopo mkoani Arusha.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, amesema kuwa moto huo umeanza kuwaka kuanzia majira ya saa 7:00 mchana, ambapo hadi sasa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  linaendelea na juhudi za kuuzima moto huo.

”Taarifa za kuteketea kwa ghala ni za kweli na hakuna madhara yoyote kwa binadamu, lakini sasa hii pamba inawaka kiaina, ukizima juu moto mwingine unaibuka chini, ukizima chini moto mwingine unaibuka juu, lakini Jeshi la Zimamoto liko hapa,  kwa pamoja tunajitahidi kuuzima. Tunaomba Mungu moto huu usienee maeneo mengine ukaleta athari zaidi”, amesema RPC Shanna.

 

Kamanda Shanna ameongeza kuwa changamoto nyingine inayowakabili ni kutokuwepo kwa vyanzo vya maji vilivyo karibu na eneo hilo ili kuweza kurahisisha zoezi la uzimaji na kwamba zoezi litakapokamilika watatoa tathmini ya hasara iliyopatikana.