HAPPINES Massawe (30), mkazi wa Pugu, Kigogo-Freshi, Dar amewatuhumu polisi kusababisha kifo cha mumewe, Mohammed Chubi (28) baada ya kumchukua katika ofisi ya Serikali ya mtaa huo alipofikishwa kwa tuhuma za wizi wa simu.
Mwanamke huyo alisema kuwa, mkasa huo ulitokea Septemba 13, mwaka huu ambapo baada ya kufikishwa kwenye ofisi hizo, difenda la polisi lilifika na kumchukua na kwenda naye Kituo cha Polisi cha Chanika, Dar.
Mama huyo ambaye ameachiwa watoto watano aliendelea kusema;
“Wakati wakiwa hapo Serikali ya mtaa, mume wangu na ndugu zake walishakubaliana kumlipa shilingi laki tatu huyo aliyekuwa akimdai hiyo simu, lakini polisi waliamua kuondoka naye.
“Baada ya kumchukua mimi na ndugu zake tulimfuatilia Kituo cha Polisi cha Chanika ambapo mimi niliweza kuzungumza naye, lakini suala la dhamana lilishindikana, tukaamua kurudi nyumbani.
“Kesho yake tuliendelea kufuatilia dhamana, lakini tukawa tunagonga mwamba wale polisi wakisema hawawezi kumuachia hadi wamalize kumhoji.
“Tulikwenda kumfuatilia mume wangu mpaka siku ya Jumatatu ambapo tulipofika kituoni hapo tuliambiwa amepelekwa gereji (sehemu maalum ya kuhoji kwa mujibu wa mwanamke huyo).
“Kuanzia hapo hatukumuona tena na kila tulipowauliza polisi walituambia anaumwa amepelekwa hospitali ambayo walikataa kututajia,” alisema mama huyo na kuongeza;
“Tukiendelea kumhangaikia, Jumatano majira ya saa 5:00 usiku, nikiwa kwenye biashara yangu ya mama lishe alikuja ndugu yangu na kuniambia kuwa mume wangu amefariki dunia.
“Hapo nikaanza kulia na kwenda kuwaeleza ndugu zake ambao walikimbilia kituoni hapo ambapo nao waliambiwa kuwa ndugu yao alishikwa na homa na kufariki dunia wakati akitibiwa hivyo mwili umehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Wale polisi waliwaambia ndugu hao kuwa kama wako tayari muda wowote polisi wawapeleke na gari yao kuwaonesha mwili huo, lakini gharama za kuuchukua na kurudi nao kwao wajigharamie wenyewe.”
Mwanamke huyo alendelea kueleza kuwa, ndugu zake walikwenda kuuona mwili huo na kabla ya kuuchukua waliomba ufanyiwe uchunguzi ambapo uchunguzi ulifanywa na daktari ambaye alitoa majibu kuwa mume wake huyo amefariki kwa presha.
“Majibu hayo yalizidi kunichanganya na kunifanya nihisi polisi ndiyo waliosababisha kifo cha mume wangu, polisi waliniambia mume wangu alifariki dunia kwa kuumwa homa na majibu ya daktari yanasema amefariki dunia kwa presha, ugonjwa ambao sikuwahi kumsikia akisema unamsumbua hata siku moja,” alisema Happines akimuomba IGP Simon Sirro aingilie kati sakata hilo.
Baada ya kuzungumza na mwanamke huyo, wanahabari wetu walizungumza na baba mzazi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Ally Mohammed ambaye alieleza jinsi alivyopokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanawe.
“Nasikitika sana ni kweli mwanangu alikuwa akidaiwa hiyo simu, lakini tukiwa pale Serikali ya mtaa tulishakubaliana kumlipa shilingi laki tatu kwa ajili ya hiyo simu, lakini wao waliamua kumchukua na kuondoka naye wakiwa huko sijui walimfanya nini mwanangu mpaka napewa taarifa za kifo chake katika mazingira ya utatanishi.
“Mbaya zaidi tulijaribu kuhangaika kumuwekea dhamana, lakini tulipigwa danadana kila tulipokwenda kuanzia hiyo Ijumaa walipomkamata mpaka Jumatano tulipopata taarifa za kifo chake,” alisema mzazi huyo.
Kwa upande wake mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Siwa Rajab alisema siku hiyo akiwa kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa huo iliyopo kwenye nyumba aliyokuwa akiishi marehemu aliwashuhudia polisi wakifika eneo hilo na kumkuta Mohammed ambaye alitii amri bila shuruti na kuondoka naye.
Alisema baada ya kuondoka naye hawakumuona tena hadi walipopata taarifa za kifo chake.
Gazeti la Ijumaa Wikienda lilimtafuta mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Mariano Maurus ambapo alipopatikana, alisema alipokea taarifa hizo kwa masikitiko japo siku hiyo hakuwepo eneo la tukio, lakini alipofika ofisini kwake alipewa taarifa za kukamatwa mwananchi huyo kisha kusikia taarifa za kifo chake ambazo alizipokea zikiwa na utata.
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi, (ACP) Zuberi Chembera ili afafanue ukweli wa tukio hilo ambapo simu yake haikuwa hewani kila ilipopigwa.
STORI: RICHARD BUKOS NA NEEMA ADRIAN, DAR