KATIKA mahojiano maalum na msichana Veronica (si jina halisi) ambaye ni mmoja kati ya wamiliki wa mgahawa mmoja uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam, tunapata kisa cha jinsi wanaume siku hizi walivyogeuka ‘wakimbizi’ katika uhusiano wao wa kimapenzi na hasa michepuko.
Veronica anasema; “Mwaka 2013 nilitoka kwetu Arusha kuja kujiunga na masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Nilipofika nilianza masomo kama kawaida.
“Nakumbuka wikiendi moja nilitoka nikiwa na rafiki zangu kwenda klabu usiku, ilikuwa inaitwa Maisha Club (Masaki).
“Tukiwa huko nilikutana na mwanaume mmoja ambaye kwa wakati huo sikuwa ninamfahamu, akaniomba namba za simu, tukawa tunawasiliana kama marafiki.”
Hata hivyo, Veronica anasema, urafiki ilikuwa ni hatua moja tu, lakini kilichofuata ni kuanza kwa uhusiano wa kimapenzi wenye mahaba na ahadi nyingi za kupendeza.
Veronica anasema ni kama aliona maisha yamebadilika ghafla, hakuwa mtu wa dhiki, mgodi ulikuwa umetema na alikuwa na uwezo wa kula anachotaka; starehe haikuwa kitu cha kuumiza kichwa.
“Baadaye aliniambia nihame kwenye chumba ambacho nilikuwa naishi na rafiki yangu maeneo na Ubungo-Maziwa, akanihamishia Sinza- Palestina,” anasema Veronica.
Hivi ndivyo wasichana wengi hasa wazuri walivyofanyiwa na wanaume wenye fedha enzi hizo za ‘mambo safi’ na jeuri ya fedha.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na OFM mwaka huu umeonesha kuwa mbwembwe za wanaume mfano wa mpenzi wa Veronica zimefifia na wengi waliokuwa wakimiliki ‘vidumu’ vya wasichana warembo wamesalimu amri kwa wake zao.
Sababu ndizo zinazotafutwa kwenye uchunguzi wetu ambapo Jamal, mkazi wa Magomeni na mfanyabiashara wa magari, yeye anasema majira yamebadilika.
“Biashara ya magari ilikuwa inalipa, tulikuwa tunapata fedha nyingi, wakati mwingine siyo kwa kuuza, lakini hata kwa kuyakodisha.”
Jamal anaeleza kuwa, kutokana na ukubwa wa kipato baadhi ya wanaume walikuwa wanaona wanaweza kufanya lolote kwa mtu yeyote, ndiyo hao waliokuwa wanawapa jeuri baadhi ya wasichana.
Leo shuhuda zimebadilika, mazungumzo mapya yamefunika kurasa nyingi za maisha ya watu ambao zamani walikuwa hawagusiki mjini kwa fedha na jeuri za; “Utanifanya nini?”
“Mwaka 2016 nilianza kuona mwenzangu anaanza kubadilika, visa vikawa vingi, ile hali ya kunidekeza tena ikaanza kupungua, akili mpya ilianza kufunguka kwamba mwelekeo wa mapenzi yetu haukuwa mzuri.
“Nilianza kujiuliza akiniacha nitafanya nini? Maana wakati huo chuo nilikuwa nimeacha kwa sababu aliniahidi kunitafutia chuo kingine nchini Kenya,” anasema Veronica, yule msichana wa Sinza- Palestina mwenye matanuzi mengi.
Kwa Veronica simulizi hii ni ya kusikitisha kwa sababu inamkumbusha jinsi alivyoyaweka rehani maisha yake kwa mwanaume ambaye alikuwa mume wa mtu na mwenye familia yake.
Hata hivyo, kila aliaye hushika kichwa chake, maana wakati Veronica anashuhudia machungu, Aminiel Tesha, mkazi wa Mikocheni jijini Dar anasema;
“Bora siku hizi na sisi wenye maisha ya chini heshima yetu imerudi.”
Kwa nini anasema hivyo?
“Enzi hizo ni msichana gani mrembo angeweza kunisikiliza mtu kama mimi? Hata wahudumu wa baa walikuwa wanachagua kuhudumia meza walizokaa wenye pesa zao sisi wenye fedha za mawazo tulikuwa tunaita huduma hadi unachoka.”
Haya ndiyo yalikuwa maisha ya ‘mupe yule, yule pale muruke’ mtu mmoja tu akiingia sehemu, basi msomi na mjuzi wa kila kitu ni yeye; achilia mbali serikalini vyeo vyote vitakuwa chini yake;
“RPC hanisumbui nafahamiana naye.”
Basi hayo ndiyo yaliyokuwa ‘maisha ya wenye meno’ ambapo ‘vibogoyo’ iliwapasa kuambulia vicheko tu hata kama waliyoyaona yalikuwa yanawakera.
Kwa nini mambo haya yamepotea kama moshi mawinguni?
Samson wa Tegeta jijini Dar anasema; fedha za kuchezea hakuna.
“Nilikuwa nina uhakika kila nikiingia kazini, wakati huo ni kibarua tu pale bandarini nilikuwa sikosi kutoka na laki mbili kila siku.
“Nilikuwa nakunywa pombe nitakavyo, yaani hata kama laki itaisha haikuwa kesi kwangu kwa sababu kesho yake nilijua napata nyingine.
“Lakini hivi sasa ukirogwa uimwage shilingi elfu ishirini utaijutia wiki nzima.”
Je, hii ni sababu ya wanaume kurudisha mpira kwa kipa na kuwa walezi wazuri wa familia, saa 2:00 usiku wako nyumbani wanaangalia taarifa za habari?
Mwasi Masanja wa Mwanza anasema; “Wanaume siku hizi wamekuwa wagumu kutoa pesa, yaani ukitaka asipokee simu yako wewe muombe hela tu.”
Dayness wa Mbezi jijini Dar, anasema yeye haoni tofauti kwa sababu hakuwahi kuishi maisha ya kutegemea mwanaume ingawa anakiri kwamba baadhi ya mashoga zake wanalia.
“Baadhi ya wasichana wanalalamika, hata rafiki zangu wameporomoka kimaisha kwa sababu maisha yao yalikuwa yanategemea kuwapiga mizinga wanaume.”
Usikose kusoma ripoti hii wiki ijayo.