
Ghana imegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha Sulemana Abdul Samed, maarufu kama mwanaume mrefu zaidi nchini humo, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 33 baada ya kupambana na matatizo ya kiafya yaliyohusishwa na ugonjwa adimu wa Marfan syndrome, unaoathiri ukuaji wa mwili na tishu zinazounga viungo.
Samed, aliyekuwa akijulikana kwa jina la utani Awuche, alifariki Jumatatu katika Hospitali ya Kufundishia ya Tamale, kaskazini mwa Ghana, alipokuwa akipatiwa matibabu ya vidonda vilivyoambukizwa kwenye miguu yake.
Kwa mujibu wa familia yake, alikuwa amelazwa hospitalini baada ya vidonda kuwa katika hali vibaya licha ya kuendelea kupata matibabu. Ingawa hali yake ilionekana kuimarika mwanzoni, baadaye afya yake ilibadilika ghafla na kusababisha kifo chake.
Kifo chake kimezua simanzi kubwa nchini Ghana, hasa katika mikoa ya kaskazini ambako aliheshimiwa si tu kwa urefu wake wa kipekee, bali pia kwa unyenyekevu, ukarimu na uvumilivu aliouonyesha katika maisha yake.

Akizungumza baada ya msiba huo, ndugu yake Sulemana Abdul Kudus alisema familia ilishtushwa na kifo hicho kwa kuwa walikuwa na matumaini ya kupona baada ya kuona dalili za afya yake kuimarika.
“Kila mtu alijua jinsi alivyokuwa mkarimu na mwenye moyo mwema. Tangu alipofariki hadi sasa, watu wengi wamekuwa wakifika nyumbani kufahamu kilichotokea,” alisema Kudus.
Familia imeeleza kuwa vidonda vilivyosababisha kulazwa hospitalini havikusababishwa moja kwa moja na ugonjwa wa Marfan, bali vinaaminika kuwa vilikuwa miongoni mwa matatizo yaliyochangiwa na hali yake ya kiafya.
Kutokana na idadi kubwa ya waombolezaji wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi yake, familia imeamua azikwe mjini Tamale badala ya kijiji chake cha Gambaga.

Samed alivutia watu wengi ndani na nje ya Ghana kutokana na urefu wake wa kipekee. Mwaka 2022, alipopimwa alikuwa na urefu wa futi 7 na inchi 4 (sawa na sentimita 223), ingawa familia yake inaamini aliendelea kukua hata baada ya vipimo hivyo.
Madaktari walithibitisha kuwa alikuwa na ugonjwa wa Marfan syndrome, ugonjwa wa kurithi unaoathiri tishu zinazounganisha viungo vya mwili na kusababisha mikono na miguu kuwa mirefu kupita kawaida pamoja na kuongeza hatari ya matatizo ya moyo, macho na mifupa.
Kutokana na hali hiyo, Samed alilazimika kuachana na ndoto yake ya kuwa dereva wa kitaalamu. Baada ya kuishi kwa miaka kadhaa katika mji mkuu wa Accra, alirejea Gambaga kwa sababu afya yake ilianza kudhoofika na kumzuia kuendelea kutimiza malengo yake.
Katika mahojiano ya awali, alieleza kuwa alianza kugundua mabadiliko yasiyo ya kawaida mwilini alipokuwa na umri wa miaka 22 akifanya kazi katika bucha jijini Accra. Alisema ulimi wake ulianza kuvimba na kumletea matatizo ya kupumua kabla mwili wake kuanza kukua kwa kasi isiyo ya kawaida.
Licha ya changamoto nyingi za kiafya, Samed hakuruhusu ugonjwa wake umzuie kuishi maisha yenye matumaini. Alibaki kuwa mtu aliyependwa na kuheshimiwa na wengi kutokana na tabia yake ya uchangamfu na moyo wa kusaidia wengine.

Jina lake la utani Awuche, lenye maana ya “Twende” kwa lugha ya Hausa, lilijulikana kote Ghana na hata kuitangaza Gambaga kwenye ramani ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ndugu yake, popote alipokwenda alijivunia kutambulisha Gambaga kama nyumbani kwa mwanaume mrefu zaidi nchini Ghana.
Katika miezi ya mwisho ya maisha yake, mfanyabiashara Ibrahim Mahama, ambaye ni kaka wa Rais wa Ghana John Mahama, alijitolea kugharamia matibabu yake baada ya kufahamu changamoto alizokuwa akizipitia. Ingawa msaada huo ulimwezesha kupata huduma bora zaidi, hatimaye alifariki kutokana na matatizo yaliyochangiwa na hali yake ya kiafya.
Sulemana Abdul Samed ataendelea kukumbukwa na wengi si kwa urefu wake pekee, bali pia kama alama ya ujasiri, matumaini na uvumilivu, akiwa amewatia moyo watu wengi kuendelea kupambana na changamoto za maisha bila kukata tamaa.