×

Mahakama yatupa ombi la Mashinji, Matiko

MAHAKAMA ya Hakimu ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Vicnent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, waliokuwa wanaiomba mahakama hiyo kusafiri kwenda nje ya nchi kwa nyakati tofauti.

Mahakama hiyo imewataka washitakiwa hao bila kujali nyadhifa zao kuwepo mahakamani kama washitakiwa wengine. Washitakiwa hao sasa watatakiwa kujitetea kwa siku tano mfululizo kuanzia Oktoba 7 hadi 11, mwaka huu na mahakama inategemea hakutakuwepo na sababu nyingine zozote zitakazosababisha kesi hiyo isianze kusikilizwa kwa muda huo.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema, safari hizo ni mambo yao wenyewe na hayahusiani na ratiba ya mahakama. Amesema kuwa, iwapo mahakama itaruhusu maombi ya washtakiwa hao kusafiri, itakuwa imefungua mwanya kwa washtakiwa wengine hivyo haitaweza maombi ya wengine.

Hakimu ameongeza kuwa, kesi hiyo ni ya muda mrefu, inalalamikiwa sana, inatakiwa kusikilizwa na kufika mwisho,  na Prof. Safari alisema wana mashahidi wengi hivyo kesi hii inahitaji kupangwa mara kwa mara kwa ajili ya kusikilizwa upande wa utetezi. Jana Wakili Prof. Abdallah Safari aliwasilisha maombi mawili mahakamani hapo ya kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7 na 8 mwaka huu kwa sababu wanahitaji kupata muda wa kutosha kujiandaa na utetezi.

Alidai kuwa wanahitaji muda wa kutosha wa kujiandaa na utetezi kwa kuwa wana mashahidi wengi ambao wanahitajika kutafutwa na kuandaliwa. Pia aliomba ruhusa ya kusafiri kwa mshtakiwa Mashinji kuanzia Septemba 26 mpaka Oktoba 6 mwaka huu kwenda Uingereza huku mshitakiwa Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini, kuanzia Septemba 25 hadi 28, mwaka huu anatakiwa kwenda Kigali nchini Rwanda na Oktoba 13 hadi 18 ambako atakwenda kuiwakilisha nchi barani Ulaya.

Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi walipinga maombi hayo yote kwa kuwasilisha hoja mbali mbali. Barua ya maombi ya kusafiri Mashinji haijitoshelezi kwani haielezi anakwenda huko kufanya nini na kwanini aende mshitakiwa huyo ambaye tarehe hizo shauri lake litatajwa mahakamani, ” alidai Nchimbi.

Kuhusu mshitakiwa Matiko, Nchimbi alidai barua ya mshitakiwa huyo inaonesha imetoka Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla) kwenda kwa Katibu wa Bunge wakiomba uwakilishi wa wabunge sita nchini Kigali.

Alidai hayo yanabaki kuwa maombi ambayo yanaweza kukubaliwa au kukataliwa na kuongeza kuwa hakuna sababu ya mshitakiwa huyo kwenda safari hiyo kwa kuwa kuna uwakilishi wa wabunge wengine watano.

Mbali na Mashinji na Matiko, washitakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa, Februari Mosi na 16, mwaka jana, Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko la kutawanyika.

Stori na Felista Masae