×

Binti Aliyefiwa Baba, Mama, Wadogo Zake Hitaji Moja

HUZUNI, machozi, rambirambi, pole ahadi za malezi kwa Anna Zambi binti aliyefiwa na baba, mama na wadogo zake watatu zimetajwa kuwa hazitoshi na kwamba hitaji moja ni muhimu kwake kwa sasa kuliko vyote. 

 

Mchungaji Innocent Kamote wa huduma ya Mission With Christ (MWC) wa Muheza, Tanga alilitaja hitaji hilo alipozungumza na Uwazi kuwa ni “faraja.”

 

“Anahitaji zaidi faraja kuliko kipindi kingine chochote maishani mwake,” alianza kueleza Mchungaji Kamote. Alisema, hata kama watu watachanga mifuko ya fedha na kumuahidi maisha bora, haitaweza kumuondolea huzuni ya kuwapoteza wazazi wake na ndugu zake hao.

 

“Umeshawahi kusikia mtu anajiua na kuacha utajiri mkubwa? Sababu ni nini ni kwamba mtu huyo alikosa faraja, alipoteza matumaini ndiyo maana akajitoa uhai. “Na binti yetu mpendwa pamoja na mambo mengine yote tunayomuahidi tusisahau kumfariji, tusiache kumuombea neema ya Mungu itakayompa matumaini mapya,” alisema mchungaji Kamote.

MWANASAIKOLOJIA ANENA

Mwanasaikolojia mahiri nchini, Chris Mauki naye kwa upande wake alizungumzia umuhimu wa Anna kujengwa zaidi kisaikolojia badala ya kuachwa aubebe mzigo mzito wa kufiwa na wazazi pamoja na wadogo zake.

Alisema: “Ukitaka kujua uzito wa hili tukio uvae uhusika, wewe ndiyo uwe Anna, utajua hiki ninachokuambia. “Vita ya mambo matatu yaani kuikataa taarifa, kubishana na ukweli na hasira, ikishika kasi ndani huleta matokeo mabaya.

“Ninachoshauri kwa watu wa karibu na Anna ni kumjenga kisaikolojia ili akubaliane na matokeo, awe na matumaini mapya ya maisha na ayaache maisha yaendelee,” alisema Mauki.

 

WENGI WALIOGOPA LILILOMKUTA ANNA

Tangu msichana huyo aliyefichwa kifo cha wazazi wake na ndugu zake awekwe wazi juu ya tukio hilo na kuonesha uchungu aliokuwa nao, watu wengi wamekuwa wakiomba yaliyomkuta yawaepuke.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete aliandika katika ukurasa wake wa Instagram:

 

“Mungu awahifadhi wazazi wetu. Tukio hili la mtoto wa marehemu rafiki yetu Zambi, aliyefariki pamoja na mkewe na watoto watatu na kumuona binti Anna aliyekuwa kwenye mitihani, kimenipa majonzi na kuniliza upya,… MWENYEZI MUNGU NIHIFADHI MIMI NA KIZAZI CHANGU.”

Aidha, wengi wamekuwa wakimuombea kwa Mwenyezi Mungu Anna ili aweze kupata ujasiri wa kulikabili tukio hilo la kusikitisha.

 

WAZIRI ATOA NENO

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu juzi (Jumapili) kwenye ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Pole nyingi kwa binti yetu Anna Zambi. Hili jambo ni kubwa mno kwa mtoto huyu. Inaumiza sana. Ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

 

“Nasi Wizara ya Afya tukiwa na dhamana ya kusimamia ustawi na maendeleo ya watoto nchini, tunachukua jukumu la kuratibu na kusimamia psychosocial support ya mtoto huyu pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wake kwa ujumla.

“Hivyo leo Katibu Mkuu Dkt. John Jingu na Kamishna wa Ustawi wa Jamii wataitembelea familia yake iliyopo Goba. Tutatoa taarifa zaidi. Tunawaombea pumziko la amani wazazi na ndugu zake Anna ambao wamepoteza maisha katika ajali mbaya. Bwana ametoa, Bwana ametwaa.”

 

PADRI ATAKA ANNA AWE KARIBU NA KANISA

Padri Carlo Mahichiro wa Kanisa la Anglikana, alisema mtoto huyo anastahili kuwa karibu na kanisa na kupewa neno la faraja na watumishi wa Mungu. “Huwezi kumuacha tu kwa imani kwamba ni mapenzi ya Mungu. Ni lazima awe karibu na watumishi wa Mungu ambao kazi yao kubwa itakuwa kumpa neno la faraja na kumsisitizia kuwa Mungu hawezi akamuacha. “Aelezwe kwamba Mungu ni lazima atatenda maajabu kwake kwa kumtimizia haja zake ambazo zingefanywa na wazazi wake.”

 

MAALIM ASISITIZA NENO LA FARAJA

Naye Mtabiri Maarufu nchini, Maalim Hassan Yahya Hussein alisema jambo lililomtokea mtoto huyo ni kubwa na kwamba walio karibu naye wanapaswa kumhubiria maneno ya Mungu.

“Kuna maandiko mbalimbali ya Mungu yanapatikana katika vitabu mbalimbali. Watu walio karibu na mtoto huyo wanapaswa kumsomea maneno hayo ya faraja na kumuonesha upendo. Hilo litasaidia katika kuweka sawa akili yake kwa sababu kilichotokea ni kitu kikubwa sana kwake,” alisema Maalim Hassan.

WAZIRI AOMBA AWE BABA WA ANNA

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, katika ukurasa wake wa Instagram alimuomba Anna aliyefiwa na wazazi wake awe baba yake wa hiyari. “Anna Zambi mwanangu: Milango ya nyumbani kwangu iko wazi kwa ajili yako muda wowote. Naomba kuwa baba yako wa hiyari. #MtotoWaTaifa #AnnaZambi.”

 

MSIBA UPYAA

Licha ya kwamba tukio lililogharimu uhai wa baba wa Anna, Lington Zambi, mama yake Wilfrida Lyomo na wadogo zake watatu, Lulu, Grace ma Andrew lilitokea takriban majuma matatu yaliyopita, lakini liliamsha hisia upya kwenye jamii baada ya binti huyo kupelekwa kuoneshwa makaburi ya familia yake.

 

Awali, Anna hakuambiwa taarifa za vifo vya wazazi wake vilivyotokea baada ya gari lao kutumbukia mtoni walipokuwa wakienda kuhudhuria mahafali yake kwa sababu walitaka afanye kwanza mtihani wa kuhitimu kidato cha nne. Aidha, baada ya kumaliza mitihani hiyo ndugu wa Anna wanaoishi Goba jijini Dar es Salaam walimweleza kilichotokea na hivyo kuibua simanzi upya hasa kutokana na binti huyo kuwaombolezea wazazi wake kwa  huzuni kubwa.

 

SIMANZI MITANDAONI

Pengine simanzi iliyokuwepo wakati wa mazishi ya familia hiyo haikuwa kubwa kama iliyotokea baada ya binti huyo kujulishwa habari za msiba.

Watu mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii waliungana na binti huyo katika maombolezo huku kila mmoja akiweka ujumbe wenye maneno ya kumtia nguvu. Kwa upande wake Zamaradi Mketema (mtangazaji) aliomba ndugu wamruhusu aishi na Anna, jambo ambalo lilipingwa. Jacqueline Wolper (mwigizaji) katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Pole sana mtoto wa Mungu aiseeeee.”

Stori: Mwandishi Wetu