×

Fiesta Dar: Kiba, Harmo Kupindua Meza Kibabe Leo

DAR ES SALAAM: Mastaa wakubwa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’, wameapa kufia jukwaani na kupindua meza ya rekodi kwenye Shoo ya Fainali ya Fiesta.

 

Shoo hiyo inatarajiwa kuliteka Jiji la Dar na viunga vyake kuanzia leo asubuhi na usiku wa kuamkia Sherehe ya Uhuru, Desemba 9 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

 

Kwa nyakati tofauti, wawili hao, wameeleza namna walivyojipanga kuhakikisha wanakonga vilivyo nyoyo za mashabiki wao wa jijini Dar na viunga vyake.

 

Novemba 26, mwaka huu, waandaaji wa Fiesta ambao ni Clouds walitangaza baadhi ya wasanii nchini watakaoshiriki tamasha hilo, wakiwemo wawili hao.

 

Kukutana jukwaani kwa wasanii hao kunasubiriwa kwa hamu kutokana na Harmonize au Harmo kuachana na Lebo ya Wasafi, hivyo mashabiki wengi kutaka kumshuhudia akitoa burudani kwenye jukwaa la waliokuwa wapinzani wake wakati akiwa Wasafi chini ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Wakati akiwa Wasafi, Harmo hakuwahi kushiriki Tamasha la Fiesta tofauti na Kiba aliyewahi kushiriki mara kadhaa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmo alitangaza listi ya nyimbo atazopafomu kwenye Fiesta kesho.

 

“Ninawaza tu pale Uwanja wa Uhuru…!!! Hiyo tarehe 8/12/2019, sijui itakuwaje maana ninapanga jiwe juu ya….!!!! Yaani sitakuwa na nafasi hata ya kunywa maji,” aliandika Harmo.

 

Alizitaja nyimbo zaidi ya 30 atakazopafomu kuwa ni Uno, Kushoto Kulia, Inabana, Niteke, Never Give Up, Atarudi, 911, Fure Waist, Show Me, Paranawe, Kadamshi, My Boo Remix, Watoto, Kwangwaru, Kainama, Oyoyo, Nikomeshe, Inde, Aiyola, Nambie, Bado, Happy Birthday, Matatizo, DM Chick, Tepete, Shulala, Nishachoka, Sina na Nionyeshe.

Kwa upande wake Kiba kupitia kwa mmoja wa mameneja wake, Esi Mgimba alisema; “Mashabiki wa Kiba wajue, huu ni wakati wa watu ku-enjoy (kufurahia) muziki mzuri kutoka kwa King Kiba.”

 

Wakati wa Tamasha la Wasafi lililofanyika kwenye Viwanja vya Posta-Kijitonyama, Dar, Mondi aliwaalika Kiba na Harmo, lakini walikataa.

 

Kwenye shoo hii ya Fiesta, jamaa hao wanatajwa kupania kwenda kuvunja rekodi ya shoo iliyowekwa jijini Dar na Mondi kupitia Wasafi.

 

STORI: NEEMA ADRIAN, Risasi Jumamosi

Leave a Comment