MWILI wa Seth Bosco ambaye alikuwa mdogo wa mwigizaji maarufu wa filamu, marehemu Steven Kanumba, umetolewa katika mochwari ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako ulikuwa umehifadhiwa na kuelekwa katika kanisa la KKKT Kimara-Temboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa ibada.

Seth aliyefariki usiku wa kuamkia juzi baada ya kuugua kwa muda, utaagwa na kuzikwa leo Desemba 9, 2019, katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wasanii waliofanya naye kazi katika tasnia ya filamu, pamoja na ndugu wa karibu, wamejitokeza katika shughuli za kuuaga mwili huo wakati shughuli za maziko zikifanyika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wahusika, maziko yatafanyika kuanzia saa 10 jioni hii.

