×

Daktari ‘Muuaji wa Vichanga’ Anaswa! – Video

ASIKWAMBIE mtu, baadhi ya matukio yanayotokea Bongo yanatisha, kuna daktari mmoja amenaswa akituhumiwa ‘kuua vichanga’ katika zahanati yake iliyopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

 

Mpango wa kumnasa daktari huyo maarufu kwa jina la Dokta Awadhi Juma (40), ulisukwa hivi karibuni kwa ustadi na kikosi kazi cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers kwa kushirikiana na polisi baada ya taarifa zake za kuwatoa wanawake mimba kwa wingi kuvuja.

 

“Yaani pale kuanzia asubuhi mpaka usiku, wanawake wamekuwa wakijipanga foleni kutoa mimba tu.

“Lakini ukifika nje ya hicho kizahanati, utakutana na bango limeandikwa wanatibu na kung’oa meno lakini yote hiyo ni zuga tu, ndani yanafanyika mauaji ya watoto kuliko kawaida. Chanzo chetu kilisema na kuomba OFM kufanya uchunguzi.

 

OFM WAANZA UCHUNGUZI

Kama kawaida OFM baada ya kupokea taarifa hizo walianza kuzifanyia kazi taarifa hizi kwa kufika kwenye zahanati hiyo kuangalia mazingira yalivyo ambapo walijionea wanawake mbalimbali wakiingia humo kwa zamu.

“Tumefika pale tumeona wanawake wengi wanaingia humo, lakini sisi hatukuingia ndani,” kachero wa OFM aliwasilisha taarifa yake kwa bosi wake aliyewatuma kufanya uchunguzi huo.

 

Aidha, baada ya kupata mrejesho huo, timu ya OFM walijiridhisha kuwa kuna jambo la ziada tofauti na huduma ya meno inayotolewa kwenye zahanati hiyo.

“Hakuna wanaume walioingia kwenye zahanati hiyo?” Bosi wa OFM aliwauliza makachero wake na kujibiwa: “Hatukuwaona.”

 

SIKU YA PILI YA UCHUNGUZI

Jumatano mchana kikosi kazi cha OFM kwa mara nyingine kilirudi tena kwenye zahanati hiyo huku kikiwa na mpango wa pili wa kuendelea na uchunguzi wake, lengo likiwa ni kuonana na daktari Awadhi kwa lengo la kujifanya kuwa mmoja kati kuwa na kusudio la kutoa mimba.

Bila kujulikana, makachero walifanikiwa kuingia kwenye zahanati hiyo na kuwakuta wasichana wengine watatu wakiwa kwenye bechi wanasubiri huduma.

 

Aidha, mmoja kati ya makachero wa OFM aliyepewa kazi ya kujifanya ana mimba alianza kulalamika mbele ya mwenzake kuhusu hofu yake ya kupatiwa matibabu bila kuyataja.

“Ila mimi sijui kwa nini naogopa namna hii?”

“Usiogope tiba shoga yangu, unafikiri usipotibiwa itakuwaje?” kachero mwenzake alimjibu.

 

KACHERO OFM AJIFANYA KUTAKA KUTOLEWA MIMBA

Baada ya kupanga foleni kwa muda mrefu, walikaribishwa na msaidizi wa kike wa dokta Awadhi ambaye walimwambia aina ya tiba wanayotaka ni kutoa mimba.

“Anakuja sasa hivi mtaongea naye,” alisema msaidizi huyo wa dokta Awadhi ambapo baadaye walifanikiwa kukutana naye na walipomuambia kuwa wanataka kutoa mimba hakusita kuwapa huduma hiyo.

 

ONJA MAZUNGUMZO YA OFM NA DOKTA AWADHI

“Ina miezi mingapi?

“Ina miezi mitatu na nusu dokta.”

 

“Sawa sh 500,000 zipo?

“Mbona hela nyingi hivyo dokta.. jamani nisaidie mimi mwenzio baba ataniua?”

“Kweli dokta msaidie dada yangu, baba atatufukuza nyumbani,” OFM mwingine alichombeza huku wote wakijifanya kuwa wametoka familia bora kimaisha.

 

DOKTA ATAKA LAKI TATU

Baada ya mapatano ya muda mrefu kati ya makachero na dokta Awadhi, walikubaliana kuwa huduma hiyo ya kutoa mimba itafanyika kwa kiasi cha shilingi 300,000 siku iliyofuata saa 4 asubuhi.

 

“Basi twenda dada yangu tukampige fiksi baba atupatie fedha hiyo,” kachero mdogo alimwambia mwenzake na kisha kutoka chumbani kwa daktari huyo huku wakiwa wamepata vielelezo vyote vya sauti na picha ya mazungumzo yao.

 

ALIYETOLEWA MIMBA TATU AJITAPA KWA OFM

Hata hivyo, makachero hao wa OFM walipomaliza mapatano na dokta Awadhi hawakuondoka, waliketi tena kwenye benchi ili kuwachunguza wanawake watatu waliokuwepo hapo walifuata huduma gani pale.

 

Maongezi kati yao yaliponoga huku foleni ikiendelea mwanamke mmoja alianza kujitapa kutoa mimba tatu kwa dokta huyo bila kujua kuwa naye alikuwa akirekodiwa na kupigwa picha kwa siri.

“Mmmh, shoga nilikusikia pale unapomwambia mdogo wako sijui unaogopa, nikuambie kitu? We wala usiwe na wasiwasi, mimi huyu dokta keshanitoa mimba mara tatu na wala sijapata tatizo lolote.”

 

WENGINE NAO WAMWAGA SIRI

Wakiwa hawajui kama wanazungumza na makachero wa OFM, wanawake wengine nao walianza kutoa siri zao kila mmoja akieleza sababu iliyomfanya afike hapo kutoa mimba.

“Mi mwenyewe nimelikoroga, mume wangu kasafari leo hii akinikuta na mimba nitamwambiaje, naitoa,” alisema mwanamke mmoja aliyekuwa akisubiri zamu yake ifike.

 

Ghafla mazungumzo kati ya OFM na wanawake hao yalikatika ghafla baada ya mwanamke mmoja kutoka chumba cha daktari huku akionesha usoni kuwa na aina ya maumivu ambayo si ya kutolewa jino kama zahanati inavyotambulisha huduma zake.

 

OFM YAUNGANA NA JESHI LA POLISI

Siku iliyofuata baada ya kukamilisha zoezi la uchunguzi wa pili na kachero wetu kuahidiwa kutolewa mimba yake feki siku ya Jumatano saa 4, taarifa za kuwajulisha polisi uwepo wa tukio hilo ilitolewa.

Kwa wepesi na umakini mkubwa jeshi la polisi lilileta kikosi kazi cha askari wa kike na wa kiume wa kutosha kwa kufanisha zoezi la kumnasa daktari huyo.

 

DAKTARI ALIVYONASWA

Makachero baada ya kuweka mtego wao na polisi kachero aliyekuwa akitolewa mimba siku hiyo alifika kwenye zahanati hiyo na kumweleza dokta Awadhi kuwa amefanikiwa kupata kiasi cha shilingi 200,000 ambazo dokta huyo alizipokea harakahara na kuziweka mfukoni mwake bila kujua kuwa namba zake zilikuwa zimerekodiwa na maofisa wa polisi.

 

HALI ILIVYOKUWA CHUMBA CHA KAZI

Dakika kadhaa ndani ya chumba cha daktari Awadhi, zilikuwa ni kama za kuweka silaha begani kabla ya kufanyika kwa mashambulizi.

Kuonesha kwamba dokta Awadhi hatoi huduma ya kung’oa meno, alimwambia kachero wetu atoe nguo za ndani.

 

“Aliniambia nitoe nguo za ndani, nikafanya hivyo, kwa kuwa nilikuwa na gauni refu nilibaki nikiwa nimejistiri vizuri tu.

“Lakini kilichonishangaza zaidi wakati nafanya maandalizi hayo alinisogelea na kuanza kunipapasa, kama mtu aliyekuwa anahitaji kufanya jambo lingine kabla ya kunitoa mimba ambayo hadi wakati huo hakuwa amenipima wala nini,” kachero wetu aliwaambia mabosi wake baada ya zoezi kukamilika.

 

CHUMBA CHAVAMIWA

Ni kama alikuwa haamini macho yake, kabla ya kufanya chochote dokta Awadhi alishuhudia kundi la watu pamoja na Mjumbe wa Nyumba kumi Mtaa wa Mpakani B, Sinza aliyejitambulisha kwa jina la Salma Maganga likiingia kwa nguvu katika chumba hicho na kumtia chini ya ulinzi.

 

ATAKA KUFANYA MAKEKE

Baada ya kunaswa Dokta Awadhi alitaka kuleta makeke na ujuaji lakini alitulizwa na maafande hao. Alipoambiwa kama alipokea pesa yeyote kwa kachero wa OFM aliyetaka kumtoa mimba alikataa.

“Jino unag’oa kwa shilingi ngapi?” afisa wa polisi alimuuliza dokta Awadh.

 

“Shilingi 10,000.”

“Kwenye mifuko yako huna fedha zenye namba hizi?” polisi alimuuliza tena.

Alipotaka kukataa tena, askari hao walimlazimisha atoe fedha alizokuwa nazo na kumkaribisha mjumbe ambapo alifanya hivyo.

 

Mara paaap noti ya kwanza ya mjumbe ilipokunjuliwa na mjumbe ikabainika kuwa ina namba ambazo polisi walikuwa wanazitaja, hapo ndipo dokta Awadhi jasho lilipomtoka.

“Nisameheni jamani mimi ni baba wa familia, mtaniharibia maisha ndugu zangu,” dokta Awadhi aligeuka kuwa mpole.

 

AMTAMBUA MPIGAPICHA WETU

Baadaye dokta Awadhi alimtambua mwandishi wetu na kumuomba amsaidie kuzima soo hilo kwani tayari lilikuwa limemkalia vibaya.

“Dah, kumbe na wewe ndugu yangu upo? Nisaidie kaka, naniii yuko wapi (anamtaja mwandishi mwingine) aisee nisaidieni jamani.”

 

MADAI YA KUUA VICHANGA ZAIDI 200 YATOLEWA

Mapema kabla ya kufanyika zoezi la kumkamata vyanzo vya habari vilisema kuwa huwenda daktari anawatoa mimba wanawake 10 kila siku kwa jinsi wanavyomiminika kwenye zahanati yake.

Ikiwa hesabu hiyo itathibitika basi dokta Awadhi ‘anaua watoto’ zaidi ya 200 kwa mwezi.

 

ASOMBWA MPAKA KITUONI

Aidha, baada ya kubambwa Daktari huyo mbele ya makachero wetu alikiri kufanya unyama huo wa kuwachoropoa mimba wanawake kinyume na sheria za nchi yetu.

Kutokana na tuhuma hizo askari walimsomba daktari huyo na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa ajili ya mahojiano zaidi.

 

RPC ATAFUTWA

Kufuatia sakata hilo mwanahabari wetu alimpigia simu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP) Mussa Taibu ili kujua kilichoendelea katika sakata hilo ambapo simu ya kamanda huyo haikuwa hewani kila ilipopigwa.

 

Kikosi kazi cha OFM kinaendelea kufuatilia tukio hili na kwamba kile ninachoendelea kitakuwa kinapakuliwa kupitia vyombo vyetu vya habari.

Ili kuipata habari hii kwa undani, ingia You Tube kisha tafuta Global Tv Online.

STORI: RICHARD BUKOS (RISASI OFM)

Leave a Comment