
Klabu ya Simba SC imemtambulisha kocha wake mpya Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck jana Jumatano Desemba 11, 2019 akiwa na rekodi ya kufundisha timu mbili tu barani Afrika.
Vandenbroeck anachukua mikoba ya Patrick Aussems aliyetimuliwa hivi karibuni baada ya kuiongoza Simba kutwaa ubingwa Ligi Kuu pamoja na kufuzu kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Kocha Sven amewahi kufundisha timu ya Taifa ya Zambia pia alikuwa kocha msaidizi wa Cameroon akiwa hana rekodi ya kuifundisha klabu yoyote barani Afrika.

MBELGIJI NI NANI?
Ana miaka 40 tu. Anaonekana kuwa na uzoefu kwenye soka la Afrika kwani
mwaka 2017 alikuwa Kocha Msaidizi wa Cameroon iliyotwaa Kombe la Afrika. Bosi wake alikuwa Hugo Broos ambaye naye Mbelgiji. Mwaka jana akapewa mkataba wa muda na Zambia kuiongoza kwenye mbio za kufuzu fainali za Afcon mwaka huu Misri, akakwama na baadae hawakumuongezea. Zambia ilimaliza na pointi saba na kuwa ya mwisho kwenye kundi lake. Kocha huyo anafahamiana vilivyo na kiungo staa wa Simba, Clatous Chama kwani wamekuwa pamoja kwenye timu ya Taifa
ya Zambia. Mbali na hizo, amewahi kucheza kwa kipindi kirefu kama beki na baadaye kuzifundisha Niki Volos ya Ugiriki na Oud Leuven ya Ubelgiji. Kocha huyo jana alikutana na msaidizi wake, Seleman Matola jijini Dar es Salaam na leo atatembelea mazoezi ya Simba kwenye Viwanja vya Mo Simba Arena, Bunju na kusalimiana na wachezaji wakati akisubiri kibali cha kazi. Kocha huyo ana mechi tatu mkononi kabla ya kukutana na Yanga ya Boniface Mkwasa.