
MECKY Maxime tayari ni kocha msaidizi wa Yanga na kilichobaki mpaka sasa ni kutangazwa tu rasmi na uongozi wa timu hiyo.
Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa Yanga ilikuwa ikisaka kocha msaidizi mzoefu ambaye atasaidiana na kaimu kocha mkuu, Charles Mkwasa kuhakikisha Yanga inarejea kwenye mstari wake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema kuwa, uongozi wa timu hiyo ulikuwa kwenye mchujo mkali wa kupata kocha msaidizi ambapo kulikuwa na majina ya makocha wawili ambao ni Kalimangonga Ongalla na Maxime.
Baada ya mchakato mzima kufanyika kwa kina, ndipo Maxime ambaye ni kocha wa Kagera Sugar akapitishwa na tayari wamekubaliana kila kitu huku akisaini mkataba wa miaka miwili na sasa kinachosubiriwa ni uongozi kumtambulisha rasmi.

“Watu wengi naona wamekuwa wakiisifia sana Simba kwa kumpatia nafasi Selemani Matola ya kuwa kocha msaidizi huku wakisahau kwa upande wetu kama nasi tayari tumeshamalizana na Maxime ambaye atakuwa kocha msaidizi kwa Mkwasa.
“Tunamshukuru sana Mkwasa ambaye kwa namna fulani ndiye aliyehusika kwa asilimia kubwa ya kumpata Maxime, kwani awali alipoombwa na uongozi kutafuta msaidizi aliwekeza nguvu zake nyingi kwa Ongalla ila baada ya kuona mawasiliano yanakuwa magumu alihamishia nguvu zake kwa Maxime, ambaye tumefanikiwa kumalizana naye,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela simu yake haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa Maxime lakini Championi limejiridhisha kwamba dili limeisha.
Musa Mateja Dar es Salaam