×

Watatu Mbaroni Mauaji ya Bodaboda

MANYARA: Jeshi la Polisi Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, limewatia mbaroni watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa pikipiki (bodaboda), Shabani Ally (21), mkazi wa Kijiji cha Bwawani.

 

Katika tukio hilo lililojiri wilayani humo hivi karibuni, Polisi waliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kidevu Mohamed Kidevu (22), Noel Mfundo (22) na Wedi Leganga (40).

 

Polisi walisema watuhumiwa hao walikamatwa maeneo tofauti wakiwa na simu ya marehemu na pikipiki yake waliyompora ambapo awali walimwita wakijifanya wanataka usafiri kisha kumuua na kutoweka na pikipiki hiyo.

 

Polisi walisema walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao baada ya kuwafuatilia kwa njia ya mtandao kwani walikuwa wakitumia simu ya marehemu waliyompora.

 

Mkuu wa Wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa alisema, baada ya watuhumiwa hao kutiwa mbaroni, kifuatacho ni sheria kuchukua mkondo wake kwani watuhumiwa hao walikiri kuhusika na tukio hilo.

 

“Kumejitokeza mauaji ya rejareja ya watu wanne hapa Kiteto katika kipindi kifupi, watu wawili wamepoteza maisha huko Kijiji cha Kijungu, yaani mtu mmoja alijitokeza na kumchoma kisu mwenzake kisha naye akauawa na wananchi.

 

“…Mwingine ni mwenyekiti wa kamati ya mazingira, Kijiji cha Ngeju ambaye alikatwa mara mbili kichwani kwa shoka akiwa nyumbani kwake na mwingine ni huyu

Shabani (bodaboda) aliyeuawa kwa mapanga,” alisema mkuu huyo wa wilaya kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

 

Katika kikao hicho, mkuu huyo wa wilaya aliagiza watendaji wa vijiji na kata kulinda amani kwa nguvu zote katika maeneo yao ili kupunguza madhara kwa wananchi yakiwemo mauaji yasiyo ya msingi.

“Haya mauaji siyo ya lazima… wakati mwingine watendaji wetu wanatakiwa kuwa imara kwenye maeneo yao kwa kusimamia amani na kutatua matatizo ya watu kwa wakati hasa wanapogombana,” alisema DC Magessa.

Stori: MOHAMED HAMAD, Ijumaa

 

GOOD NEWS: WAZIRI KAMWELWE Atangaza Neema kwa Wafanyabiashara Bukoba

Leave a Comment