
WINGU zito limetanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambao sasa umeanza kukitikisa chama hicho na kukilazimu kuanza harakati za kuwashughulikia wale wanaokwenda kinyume na taratibu za chama. IJUMAA WIKIENDA limedokezwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya chama hicho kupitia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kikielekeza kamati yake ya Ulinzi, Usalama na Maadili kuwahoji wanachama wake watatu, Makatibu Wastaafu, Yusuf Makamba na Abdulrahaman Kinana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kuhojiwa.
Kinana na Makamba, wanapaswa kuhojiwa na kamati hiyo, kufuatia madai ya NEC kuwa wamekidhalilisha chama hicho na kiongozi wake mkuu, Rais Dk John Pombe Magufuli.
Desemba 13, mwaka huu, Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole, alieleza kuwa, viongozi hao waandamizi, wataitwa mbele ya kamati hiyo, kujibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili.
Kuibuka kwa sakata hili kumekuja kufuatia kuvuja kwa mazungumzo yao kwa njia ya simu, wakimtuhumu Rais Magufuli, kumkumbatia mtu anayejiita, mwanaharakati huru, Cyprian Musiba.
Kinana na Makamba, walikwenda mbali zaidi, baada ya kuamua kuandika barua kwa Katibu wa Kamati ya Wazee ya chama hicho, Pius Msekwa, kulalamikia vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Membe alikiri kudukuliwa sauti yake, ingawa hakuwasilisha malalamiko yoyote kwa chama chake, badala yake aliamua kumfungulia mashitaka Musiba.
…URAIS WA MEMBE
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa, kuibuka kwa wito huo, kunamlenga moja kwa moja Membe kutokana na kudaiwa kuwa na harakati za kutaka kutimiza ndoto yake ya kuwania urais.
Mwanadiplomasia huyo mashuhuri, amekuwa akitajwa kwa kasi katika siku za hivi karibuni, kufuatia madai kuwa amepanga kujitosa katika mbio za urais mwaka 2020 kupitia chama hicho.
Ingawa Membe mwenyewe hajaweka wazi jambo hilo, lakini watu walio karibu naye wanasema; ‘liwe jua au inyeshe mvua,’ ni lazima atajitosa katika kinyanganyiro hicho.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk George Kahangwa anasema hakuna sababu ya kumsimamisha Membe asiendelee na harakati zake za urais kwa sababu kugombea urais ni haki yake ya kikatiba.
Alisema iwapo kamati itabaini kuwa hilo ndilo kosa lake, haipaswi kumpa adhabu na badala yake imfafanulie tu taratibu za chama kuwa ndani ya CCM humuachia vipindi viwili rais aliyepo madarakani.
“Haitarajiwi kuwa 2020 akasimama mgombea mwingine badala ya Magufuli, ndani ya chama watamwambia kuwa utaratibu wa chama ndiyo huu, watamshauri tu kwamba asubiri 2025.
“Kama yapo matatizo mengine hayo sasa ni ya kwao, washughulikie kwa taratibu zao. Hiki chombo kisiwe mahakama, kiwe chombo cha kusikiliza wenye mawazo tofauti. Kumsikiliza kwa jicho la busara kutasaidia zaidi,” alisema.
Licha ya ushauri huo, suala la urais wa Membe pia limewahi kukemewa na Katibu Mkuu CCM, Dk Bashiru Ally kuwa Membe amekuwa na mwenendo wa kutia shaka ndani ya chama hicho na kumtaka afike ofisi za chama hicho jijini Dar kujitetea na tuhuma zinazomkabili.
MEMBE AFUNGUKA
Hata hivyo, Membe ambaye duru za ulinzi na usalama zinabainisha kuwa kwa sasa ni mshauri wa masuala ya usalama wa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa tangu Desemba 2017, juzi aliitikia wito uliotolewa na CCM.
“Kutokana na wingi wa messages, nashindwa kumjibu kila mtu aliyeniandikia ujumbe kuhusu tangazo la kuitwa kwangu kwenye kamati ya maadili. Niseme tu kwamba; nasubiri kwa hamu barua ya wito! Nitakwenda! Hoja zitatolewa na hoja zitapanguliwa. Stay tuned,” aliandika Memba kwenye ukurasa wake wa Twitter.
…VIGINGI VYA URAIS
Hii si mara ya kwanza kwa Membe kuitwa na Kamati ya Ulinzi, Usalama na Maadili kuhojiwa kwani Februari, 2014, alihojiwa kwa tuhuma za kuanza kampeni mapema za urais na baadaye kufungiwa kujihusisha na siasa kwa miezi 17.
Makada sita wa chama hicho akiwa Membe ambao walikuwa kwenye mpambano wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, walikutana na rungu hilo.
Makada waliofungiwa wakati huo ni Membe, mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, Steven Wassira, January Makamba na William Ngeleja.
Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa adhabu dhidi ya Membe inaweza kuwa kubwa kama Rais Magufuli alivyowahi kunukuliwa hivi karibuni baada ya kutangaza kuwasamehe Makamba, Ngeleja na Nape.
Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM alisema alifikiria kuwa asingewasamehe wabunge hao adhabu yao ingekuwa kubwa watakapofikishwa mbele ya kamati ya maadili ya CCM, lakini kwa kuwa Membe, Kinana na Makamba hawakuomba msamaha na matokeo yake wamefikishwa kwenye kamati hiyo.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaona kuwa Membe ndiye atakayeathirika zaidi na adhabu yoyote itakayotolewa dhidi yake kwa kuwa itaweza kukwamisha mbio zake za urais ilihali makatibu hao wastaafu wakiwa hawana cha kupoteza.
Kigingi kingine ni historia kuonesha dhahiri kuwa waliowahi kujaribu kuwatikisa marais waliopo katika uongozi, walishindwa baada ya kuzuiliwa na CCM.
Membe anafananishwa na makada maarufu kama Edward Lowassa na Gharib Bilal katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Ikiwa ni miaka miwili baada ya kujiuzulu uwaziri mkuu, Lowassa alitajwa kuwa kwenye mikakati ya chinichini kupambana na Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi ndani ya CCM mwaka 2010.
Hata hivyo, Kikwete alipitishwa na kushinda, lakini Lowassa hakugombea ndani ya chama.
Naye mwanasiasa mkongwe visiwani Zanzibar, Dk Gharib Bilal alijitokeza ndani ya CCM kwa upande wa Zanzibar akitaka kumrithi Amani Abeid Karume, mtoto wa rais wa kwanza visiwani humo, Abeid Karume.
Ikumbukwe, wakati Bilal akijitokeza, Karume alikuwa ametumikia miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa visiwani humo.
Hata hivyo, Membe amekuwa akipambana na makada wa CCM wanaomtaka asigombee urais 2020 akiwemo mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni kada wa chama hicho, Rostam Aziz ambaye alimtaka Membe amuachie Magufuli 2020.
Membe alimtaka Rostam aishauri Serikali kuhusu masuala ya kiuchumi kwa sababu ndiyo fani yake na si masuala ya kisiasa.
Stori: Gabriel Mushi, DAR