
Mwanadada aitwaye, Halima Juma Ally (23) mkazi wa Chalinze Mkoa wa Pwani, amepandishwa kizimbani leo katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke akikabiliwa na mashtaka matatu ya wizi wa kimtandao.
Akisomewa hati ya mashtaka na wakili wa Serikali, Gabriel Kamugisha ameieleza mahakama kuwa shitaka la kwanza nila kuiiba kadi ya ATM ya CRDB, mali ya Erenest Mika Sakawa eneo la Mbagala Dar Live ambapo wakili huyo ameeleza kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 23 mwaka huu.
Shtaka la pili linalomkabili, Halima, ni kuiba 2,030,000, katika tarehe hiyohiyo mali ya, Erenest Mika Sakawa katika eneo la Mtoni kwa Azizi Ally akijua ni kinyume cha sheria.

Pia wakili huyo amedai katika shitaka la tatu mshitakiwa aliiba shilingi 2,000,000/= Mali ya Erenest Mika Sakawa katika tarehe hiyohiyo eneo la Keko Bora. Baada ya kusomewa mashitaka hayo hakimu alimuuliza kama ni kweli ama laa! Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na mwendesha mashtaka alieleza mahakama kuwa upelelezi katika kesi hiyo haujakamilika na akaiomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hyo, Godfrey Rwekiti amedai makosa hayo yanadhaminika na hivyo dhamana yake iko wazi ambapo mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili watakao saini bondi ya Million 2 kila mmoja ambao ni watumishi wa Serikali. Mshitakiwa hakukidhi masharti hayo na amepelekwa segerea.
Ikumbukwe kuwa mwanadada huyo alitajwa wiki iliyopita na Kamanda wa Kanda Maalumu Dar es Salaam Lazaro Mambosasa kuwa mwanamke huyo alikamatwa katika benki ya CRDB Tawi la Mbagala na askari aliyekuwa zamu baada ya kumtilia shaka.
Mambosasa alisema kuwa mwanamke huyo alikuwa akijifanya kuwasaidia wazee ndani ya chumba cha mashine ya ATM huku akijua alikua akiwalaghai na kuchukua namba zao za siri na kisha kuwabadilishia kadi.