×

Sakata la Kuzima Laini za Simu, Serikali Kupoteza Mapato

 

DAR: Wakati zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kumalizika kwa muda kusajili laini za simu kwa alama za vidole, imebainika kuwa Serikali ipo hatarini kupoteza mapato kwa kuwa zaidi ya nusu ya wamiliki wa laini za simu nchini hawajasajili laini zao kwa alama za vidole.

 

Hali hiyo inatokana na kusuasua kwa zoezi la upatikanaji wa namba za kitambulisho cha Taifa (NIDA) ambalo linakwamisha usajili wa laini hizo kwa alama za vidole.

Pia hatari hiyo inasababishwa na hamasa ndogo ya usajili wa laini hizo hali inayochangia zaidi ya laini milioni 5.6 kutosajiliwa licha ya wamiliki wake kuwa na namba za NIDA.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya usajili hadi kufikia Disemba 10 mwaka huu, Mkurugenzi wa mambo ya kisekta wa TCRA, Dk. Emmanuel Manaseh alisema kati ya laini milioni 47 zinazotumika sasa na kumilikiwa na watu milioni 21.1, laini milioni 21.7 zinazomilikiwa na watu milioni 10 hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

 

Alisema laini milioni 19.6 sawa na asilimia 42 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 7.6 ndizo zilizosajiliwa.

Aliongeza kuwa laini ambazo wamiliki wake wana namba za utambulisho NIDA lakini hazijasajiliwa ni milioni 5.5 ambazo wamiliki wake ni milioni tatu.

 

Kutokana na hali hiyo, Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Mawasiliano nchini inaweza kupoteza mapato kwa kuwa laini hizo milioni 21.1, licha ya kutumika kuingiza mapato kutokana na huduma za sauti na intaneti pia zinatumika katika miamala mbalimbali ya kifedha nchini na kuchangia pato la Taifa.

 

Ukuaji wa pato la sekta ya mawasiliano

Matumizi ya simu nchini yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na kulichangia pato la Taifa kwa nyanja mbalimbali ikiwa miamala ya fedha kwa kupitia kampuni zinazotoa huduma hizo kama vile, Mpesa, Tigopesa, Halopesa, TTCLpesa na Airtel money.

 

Hayo yanadhihirishwa na taarifa ya TCRA kwa miezi sita iliyopita ambayo inaonyesha miamala ya zaidi ya Sh trilioni 16 ilifanyika mpaka Juni mwaka huu.

 

Mamlaka hiyo inasema kwa robo ya kwanza iliyoishia Machi 30 mwaka huu, miamala milioni 243.52 iliyofanyika ilikuwa na thamani ya Sh trilioni 7.82 huku miamala milioni 260.43 iliyofanyika kati ya Aprili na Juni ilikuwa ya Sh trilioni 8.31.

 

Lakini pia kuanzia mwaka jana, TCRA ilikuwa ikitoza gharama za mawasiliano ya simu kwa shilingi 15.60 kwa dakika.

 

Hii ina maana kuwa wateja hao zaidi ya milioni 10 ambao walikuwa wakitumia laini zao kufanya miamala na kufanya mawasiliano, sasa laini zitafungwa na kuleta mtikisiko katika makusanyo ya mapato ya mamlaka hiyo.

 

Ukuaji wa mapato ya sekta ya mawasiliano nchini pia unadhihirishwa na ongezeko la kasi la gawio TCRA kwa serikali ambapo mwaka 2016/17 ilitoa gawio la Sh bilioni 13.2, mwaka 2017/18 ikatoa gawio la Sh bilioni 22.3 na mwaka 2018/19 ikatoa gawio la Sh bilioni 85.5

 

Ongezeko hilo limechangiwa na ongezeko la watumiaji wa laini hizo kutoka milioni 39.8 mwaka 2015 hadi kufikia milioni 47 mwaka huu.

 

Hatari ya kupoteza mapato

Mbali na zoezi hilo kuhatarisha mapato ya serikali, pia kampuni za simu zipo hatarini kupoteza mapato yake kama alivyowahi kubainisha Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Vodacom, Hisham Hendi ambaye alikiri huduma ya miamala yaani M-pesa ni miongoni mwa huduma muhimu inayoiingizia mapato kampuni hiyo, lakini kuna changamoto.

 

“Tunaendelea kuwasajili wateja wetu kwa alama za vidole ili kutii sheria, lakini changamoto iliyopo ni gharama za kufanya hivyo pamoja na upatikanaji hafifu wa vitambulisho vya Taifa,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na IJUMAA, akiwamo Erick Evarist alisema urasimu uliopo katika upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa, ni mojawapo ya sababu inayofanya zoezi la usajili wa laini za simu kusuasua.

 

“Kwa sababu kama kupata kitambulisho cha NIDA inakuwa shida namna hii, ni wangapi watakuwa wamekata tamaa na laini zao kufungiwa? Hapo lazima serikali ipoteze mapato.

 

Hali hiyo pia ilionwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Kangi Lugola ambaye Novemba mwaka huu aliliambia Bunge kuwa laini ambazo hazijasajiliwa hadi Disemba 31 hazitafungwa.

 

Lakini wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe alisema serikali itakata mawasiliano kwa laini ambazo zitakuwa hazijasajiliwa hadi kufikia Disemba 31 mwaka huu.

Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa

 

Leave a Comment