
Raia wa kusini mwa nchi ya Madagascar wanakula udongo uliochanganywa na ukwaju kutokana na baa la njaa ambalo limesababishwa na ukame ulioikumba nchi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), ukame huo umeharibu zao la Mdungusu kakati ambalo linategemewa na wenyeji kwa ajili ya chakula.
Dungusu kakati ni mmea jamii ya Mpungate ambao hujulikana kama mkate wa maskini kwenye maeneo ya ukame kwani majani yake hupikwa mboga, maua, mbegu na matunda hutengenezwa siki au kuliwa yakiiva ilhali matawi yake ni lishe pia kwa mifugo.
“Tunauita udongo wenye kutuokoa katika kipindi hiki kwa sababu unawezesha ukwaju kupenya vizuri na kuleta ladha nzuyri mdomoni jambo ambalo linatusaidia kukabiliana na njaa katika kipindi hiki cha kiangazi,” alisema Doday Fandilava Noelisona mkulima mmoja wa eneo hilo.
Aliongeza kuwa “Siku hizi hatutafuti tena chakula ili tuishi bali tunatafuta mbinu za kupata kitu chochote cha kujaza tumbo,” alisema.
Shirika la chakula dunia- WFP, linasema watu milioni 1.5 kusini mwa Madagascar wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.
WFP wameongeza kuwa zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 85.8 kukabiliana na baa hilo la njaa ili kuokoa maisha ya watu hao wa Madagascar.
Aidha, imeelezwa kuwa licha ya Rais wa nchi hiyo kuwagawia chakula Septemba mwaka huu, hali imezidi kuwa mbaya.
Hali hiyo inadaiwa inaweza kusababisha vifo ya mamia ya watu waliofariki kwa njaa miaka ya 1990 ambapo miili ya watu ilizagaa barabara baada ya wale waliosalia hai kukosa nguvu za kuwazika wenzao
Stori: AMBOASARY, MADAGASCAR