×

Binti Aliye-trend Kuolewa na Babu Mzungu- “Anajua Mapenzi”

 

DAR: Baada ya kuwepo kwa kasumba ya mastaa wa kiume Bongo kuchukua na kuwa na uhusiano na wanawake wa nje ya Bongo, msanii wa kike wa Bongo Muvi, Aziza George, naye amewajibu baada ya kuolewa na kibabu cha Kizungu, Wolf Gang, raia wa Austria.

 

Aziza anatamba na filamu ya Msala wa Beki Tatu.

Aziza hivi karibuni alifunga ndoa hiyo na mwanaume huyo ambapo amewaomba vizabizabina kuacha kumsakama, kisa ameolewa na kibabu.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la IJUMAA, Aziza alisema anawashangaa wanaomsakama kwenye mitandao ya kijamii kuwa ameolewa na mtu mzima na hajafuata kingine bali pesa.

Aziza amesema si kweli kwamba alijuana na mwanaume huyo tangu mwaka 2012, yapata miaka saba sasa.

 

“Ni kweli nimeolewa na mtu mzima, lakini nashangaa kwenye mitandao ya kijamii watu wanachukua picha zangu za harusi kwenye akaunti yangu kisha wanazisambaza wakinizungumzia mimi, eti nimeolewa na kibabu kwa ajili ya pesa.

 

“Ukweli ni kwamba mwanaume huyu ni mtu wangu tangu mwaka 2012.

“Kuna kipindi tulipotezana hapo katikati kwa muda fulani, lakini baadaye tulikutana tena na kuamua tufunge ndoa,” alisema Aziza mwenye umri wa miaka 35 wakati mwanaume huyo ana umri wa zaidi ya miaka 60.

 

Aziza aliongeza kuwa, anampenda mno mumewe huyo kwani walipopotezana kwa takriban miaka mitano iliyopita, aliingia kwenye uhusiano na mtu mwingine na akazaa naye mtoto wa kike.

Hata hivyo, Aziza alisema kuwa, alipokutana tena na Wolf ndipo akaamua kuwa naye kwani anampenda na kumhudumia mwanaye aliyezaa na mwanaume mwingine.

 

“Baba wa mtoto wangu hamjali mtoto wala hajamuona muda mrefu, lakini tulipokutana tena na Wolf kwa kweli alifurahi sana kuniona na akakubali kumlea mtoto wangu na sasa hivi yupo kwenye hatua ya kumuasili mtoto wangu ili awe wa kwake,” alisema Aziza.

 

Msanii huyo aliongeza kuwa, watu waondoe imani potofu kuwa, unapokuwa na Mzungu unatafuta pesa, jambo ambalo siyo kweli kwa upande wake kwani yeye amefuata mapenzi kwa jamaa huyo.

 

“Ni hivi, mimi na Wolf tutakuwa wote mpaka Mungu atutenganishe maana hatuna mpango wa kuachana leo wala kesho na kingine sijafuata pesa kwake, nimefuata mapenzi ya kweli,” alisema Aziza.

Stori: Imelda Mtema

 

Leave a Comment