
STRAIKA wa Barcelona, Luis Suarez alimpiga busu maridadi mkewe Sofia Balbi hadharani wakati wakisherehekea miaka 10 ya ndoa yao juzi nchini Uruguay.
Katika sherehe hiyo, Suarez alipewa kampani na nyota mwenzake wa Barcelona, Lionel Messi ambaye alisafiri pamoja na mkewe Antonella kwa ajili ya shughuli hiyo.
Nyota wa zamani wa Barcelona, Neymar naye alikuwepo na akapiga picha ya pamoja na Messi na Suarez na kukumbushia ule utatu wao uliotikisa dunia wa MSN.
Suarez, 32, na mpenzi wake wa tangu utotoni, Sofia, 30, walifunga ndoa mwaka 2009 na wana watoto watatu pamoja.
Suarez aliwaambia waandishi “Ni siku muhimu sana kwetu “ kabla ya kutania: “Mke wangu ni beki mgumu zaidi, mtu ambaye siwezi kuondoka kwake.”
Nyota huyo wa zamani wa Liverpool aliongeza: “Nikiwa na miaka 15, nilimpata mpenzi ambaye alituliza kichwa changu. Alinisaidia kujua jinsi soka lilivyo na umuhimu kwangu.
“Nilikuwa natoa out usiku, sikufurahia kusoma na sikuwa nimejitoa kikamilifu kwenye soka. Alinipa ujasili na kunifanya nijiamini sana.”
MONTEVIDEO, Uruguay