×

Mbeya: Jeneza Latelekezwa Sokoni, Mbele ya Duka – Video

WANANCHI wa eneo la Soko la Soweto wameuanza mwaka kwa taharuki ya aina yake baada ya kuamka asubuhi siku ya mwaka mpya na kukuta jeneza tupu likiwa limetelekezwa juu ya meza nje ya duka katika eneo hilo.

 

Tukio lililofungua mwaka 2020 la kutelekezwa jeneza sokoni, limeibua maswali miongoni mwa wananchi.

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa jeneza hilo lilikuwa limetumika na wana wasiwasi kuwa aliyefanya tukio hilo ni mtu anayejihusisha na imani za kishirikina.

 

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Oscar Kilasi, ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wa soko hilo, alisema aliwahi asubuhi sokoni hapo kwa ajili ya kufungua biashara yake ya samaki na alipofika sokoni hapo alishangaa kuona jeneza kubwa likiwa juu ya meza mbele ya duka lililo jirani na duka lake, hali iliyomshangaza na kuamua kuwaita walinzi wa soko hilo kuwauliza.

 

“Nilimuita mmoja wa walinzi wetu wa hapa sokoni ambaye alikuwa anaingia ndani ya soko akasema hajui chochote na wakati tukiendelea kuulizana na kushangaa ndipo umati wa watu nao ukaanza kusogea kushuhudia tukio hili la ajabu,” alisema Kilasi.

 

Naye Kefas Nkonde, mkazi wa Ilemi, jijini Mbeya alisema, tukio hilo linatisha kwa vile sio kitu cha kawaida jeneza kuonekana sokoni na kuiomba serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo.

 

“Jeneza sio mzinga wa nyuki kwamba tutapenda kuangalia, bali ni kitu kinachoogopesha jamii, hivyo linapoonekana katika maeneo ambayo halitarajiwi kuwapo ni vizuri serikali ikafanya uchunguzi wa kina kujua kiini cha uwapo wake mahali hapa,” alisema Nkonde.

 

Alisema wanachoelewa ni kwamba kwa imani ya Wakristo jeneza linapaswa kuzikwa pamoja na marehemu na kwa utamaduni wa Waislamu jeneza halizikwi, lakini linahifadhiwa msikitini.

 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Soweto, Ramadhan Tavee, alisema tukio hilo limewashtua wananchi wake kwa vile sio la kawaida, na kwamba kinachoshangaza zaidi limetelekezwa mbele ya duka ambalo mmiliki wake anauguza mgonjwa hospitalini.

 

Alisema baada ya kuona tukio hilo aliamua kuwasiliana na viongozi wake wa juu katika ngazi ya kata kabla hajapiga simu polisi kwa ajili ya kuomba msaada wa ulinzi katika eneo lake.

 

“Nilipopata taarifa hii kama kiongozi nilifika mahali hapa mara moja kujiridhisha na niliona jeneza hili, niliwasiliana na viongozi wangu wa kata kisha nikapiga simu polisi na ninashukuru maana askari wamefika kwa wakati na kuhakikisha mtaa wangu unaendelea kuwa na amani na utulivu,” alisema Tavee.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Soko la Soweto, Fred Mwaiyongano, alisema baada ya kuliona jeneza hilo aliamua kufuatilia kwa kina ili kujua limefikaje sokoni hapo kwa sababu sio jambo la kawaida na halijawahi kutokea.

 

Alisema aliwauliza vijana wanaoshusha mizigo kwenye magari sokoni hapo na wakamweleza kuwa jeneza hilo lilishushwa na gari moja la mizigo aina ya Fuso lililokuwa limepeleka nyanya sokoni hapo likitokea katika mji wa Makambako mkoani Njombe.

 

“Tuliwasiliana na wapakiaji wa mizigo wa Njombe wakasema jeneza hilo lilitumika kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Mbeya kwenda Makambako na lilitakiwa kurudishwa Mbeya na ndipo wakalipakia kwenye Fuso hilo ili walipeleke kwenye msikiti mmojawapo uliopo Sokomatola, jijini Mbeya,” alisema Mwaiyonga.

 

Alisema vijana hao walieleza kuwa wakati wa kushusha nyanya sokoni hapo dereva alilisahau katika eneo hilo badala ya kulipeleka eneo alilokuwa ameelekezwa.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu za jeneza hilo kutelekezwa sokoni hapo.

 

Alisema mtu mmoja tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi kusaidia uchunguzi wa tukio hilo na akawataka wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi unafanyika.

Leave a Comment