
WATU watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya watu wenye silaha wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kuteka nyara basi la abiria katika kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya.
Irungu Macharia, Kamishna wa Kaunti ya Lamu amethibitisha kutokea shambulizi hilo na kubainisha kuwa, basi hilo la abiria lilikuwa linatokea mjini Mombasa likielekea Lamu kabla ya shambulizi hilo.
Inaarifiwa kuwa, watuhumiwa wa kundi la al-Shabaab wamefanya shambulizi hilo la kushtukiza katika eneo la Nyongoro lililoko karibu na wilaya ya Witu, kaunti ya Lamu.
Mapema mwezi uliopita, watu 10 waliuawa katika shambulizi jngine dhidi ya basi la abiria lililofanywa na genge la kigaidi la al-Shabaab katika kaunti ya Wajir, kaskazini mashariki mwa Kenya mpakani na Somalia.