MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Cham Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho na rais wa sasa, John Magufuli, amesema kuwa jimbo la Kawe limekuwa kama yatima kwani limekosa uwakilishi thabiti ndani ya bunge kwa kipindi cha miaka 10 hivyo kuendelea kuwa nyuma kimaendeleo.
Magufuli amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 14, katika Viwanja vya Tanganyika Packers wakati akifanya mkutano wake wa kampeni kwa majimbo ya Wilaya ya Kinondoni ambayo ni Kawe (lililokuwa chini ya Halima Mdee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema) na Jimbo la Kinondoni lililokuwa chini ya Maulid Mtulia (CCM).
“Tarehe ya leo ni siku ambayo tunamkumbuka Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kwa vijana wenye miaka 21, hawawezi kuelewa, miaka 21 iliyopita tulikuwa na muasisi wa Taifa hili ambaye ndiye aliyetusaidia kupata uhuru bila kumwaga damu.
“Baba wa Taifa ametawala, akaja Mwinyi akatawala miaka kumi hatukumwaga damu, Mkapa hatukumwaga damu, Kikwete hatukumwaga damu na mimi katika miaka yangu mitano niliyotawala sikumwaga damu, amani ni kitu kikubwa sana, usiombe vita.
“Jimbo la Kawe limekaa kama utumwani lina shida sana, watu wanateseka na kuna baadhi ya maeneo umeme ni tatizo, ninaomba mfanye mabadiliko ya makusudi mmedanganywa vya kutosha, Chadema nawapenda hata mkitaka nitoe alama hii hapa.
“Naomba mniletee Gwajima najua amepigwa vita mno, ndiyo maana hata ameshindwa kurefuka lakini ni kwa sababu ya ukweli wake, mwembe wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe na watoto, naomba na mimi mnichague niwe rais wenu.
“Msichonganishwe na mambo ya udini, mimi ni Mkristo lakini nimejenga msikiti Dar es Salaam, hata Chato nimejenga wa kubeba watu 5,000, msimwangalie Gwajima kwa sababu ya sura yake na mimi najua kutumbua majipu, nileteeni huyu ni ‘size’ yangu.
“Uchaguzi wa mwaka huu utatoa fursa kwa Watanzania kukataa vibaraka wa mabeberu katika nchi yetu.
“Jana Gwajima alinipigia simu na akaniambia mvua iliyonyesha imeharibu pia sehemu za Kawe, nikamwambia kesho kabla ya kwenda kwenye mkutano lazima nipite huko. Nafahamu huwa panakuwa na maji mengi, watu wanapata shida lakini sijawahi kuombwa hata siku moja kwamba, wananchi wa hapa wanapata shida.
“Nataka niwape pole wananchi wa Kawe, poleni, mmechelewa sana, nilikuja miaka mitano iliyopita kumuombea kura mtoto wa Warioba, Wanakawe mkasema tunakupa Magufuli lakin mbunge hatumpi, sikuwachukia. Mbunge mliyemchagua nilitegemea anisumbue au awasumbue mawaziri wangu.
“Kila nikiuliza mawaziri wangu ni miradi ipi imeombwa katika Jimbo la Kwe naambiwa hakuna, ilibidi miradi mingine tufanye kwa nguvu kwa kutambua jiografia ya Kawe kama Serikali, sababu waombaji hawapo, ikipelekwa bajeti bungeni wanaondoka, wanafunga midomo na platsa.
“Kazi ya mbunge ni kujenga mahusiano kati yake na mawaziri, usipojenga mahusiano huwezi kupata miradi watapata wengine walio karibu karibu, mliowachagua hapa Kawe hawakujenga mahusiano na mawaziri, ndiyo maana hakuna hata hospitali inayofanya upasuaji.
“Kawe inazidiwa na wilaya mpya ya Kigamboni ina Hospitali mbili za wilaya mpya za kufanya oparesheni, Kawe hamkumkosea Mungu mlikosea kuchagua, kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ndio kosa, ninawaomba mwaka huu muondoeni aliyekuwepo mniletee Gwajima.
“Nafahamu kampeni mbaya zinafanyawa mitandaoni kumchafua Gwajima, mambo ya udini, leo Kawe mmeanza kuingiziwa chuki aliyoikataa Baba wa Taifa, mimi hapa ni Mkristo na nilitaka kusomea upadri ukanishinda, yaani ukae bila kuoa na Mama Janeth wakati huo yupo?
“Katika mchakato wa kura za maoni aliyeongoza ni Furaha, huyu ni mtoto wa dada yangu anaitwa Asteria, kama anakataa aseme! Aliyemfuatia ni Kiziga amewahi kuwa Mbunge Afrika Mashariki, si kwamba hawafai lakini Gwajima anafaa zaidi, hawa wengine kazi zipo tu.
“Tunataka tuibadilishe Dar es Salaam, Kawe inahitaji mabadiliko makubwa, nimepita pale kila siku mafuriko hatga ukiwa umepika ugali wako unaenda na maji.
“Kwa Dar es Salaam nzima tumepanga kupunguza hii kero ya mafuriko mvua zinaponyesha, tumetenga Tsh bilioni 32, lakini baadhi ya mafuriko yanasabaishwa na sisi, unajenga kwenye ukingo wa mto unataka maji yapite wapi? Kinondoni nileteeni Tarimba,” ni baadhi ya kauli alizotoa Magufuli.

