
Kundi la Al-Shabaab limefanya mashambulizi mapema Jumapili, dhidi ya kambi ya kijeshi nchini Kenya, inayotumiwa na wanajeshi wa Marekani na Kenya. Lakini Kenya imesema imefanikiwa kuzuwia mashambulizi hayo bila madhara.
Kundi hilo la itikadi kali limeielezea kambi hiyo, karibu na mpaka wa Somalia, kama “moja ya vituo kadhaa vinavyotumiwa katika vita vya msalaba vya Marekani dhidi ya Uislamu katika kanda hiyo.”

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Luteni Kanali Paul Njuguma alisema wapiganaji walivamia tu uwanja wa ndege wa Manda na siyo kambi ya jeshi ya Simba kama ilivyodai Al-Shabaab. Uwanja huo wa kiraia pia unatumika kama lango la kuingilia kambini hapo.
“Hiyo ilikuwa propaganda,” alisema Njuguna, akipinga madai ya Al-Shabaab. Katika ujumbe wa Twitter, KDDF ilisema: “Alfajiri ya leo majira ya saa 11:30, kulikuwepo na jaribio la kuvuruga usalama katika uwanja wa ndege wa Manda. Jaribio hilo lilizuwiwa kwa ufanisi.”
“Mpaka sasa miili minne ya magaidi imegunduliwa. Uwanja wa ndege uko salama,” uliendelea kusema ujumbe huo wa Twitter. Hakujaripotiwa maafa yoyote kwa wanajeshi wa Marekani au Kenya.
Jeshi la Kenya lilisema moshi unaoonekana kwenye mkanda kutoka eneo la tukio unatoka kwenye gari la mafuta lililoathiriwa katika uvamizi huo, na kwamba moto huo umedhibitiwa “na taratibu za kawaida za kiusalama zinaendelea.”
Kambi ya Simba iliyoko Manda Bay, kaunti ya Lamu nchini Kenya ambayo Al-Shabaab ilidai kuishambulia.
Kamandi ya jeshi la Marekani barani Afrika pia ilitoa ujumbe wa Twitter, ikikiri kwamba ilikuwa inafuatilia hali hiyo, lakini haikutoa maelezo zaidi. Marekani imefanya mashambulizi kadhaa yanayoilenga Al-Shabaab nchini Somalia.
Marekani inavisaidia vikosi vya Somalia pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Afrika katika mapambano dhidi ya Al-Shabaab, ambalo lina mafungamano na mtaadao wa Al-Qaeda.
Al-Shabaab yadai kuhusika
Al-Shabaab ilichapisha picha za wapiganaji wake waliofunika nyuso wakiwa karibu na ndege iliyokuwa inawaka moto, ingawa picha hizo hazikuweza kuthibitishwa na wachambuzi huru.
“Ndege saba na gari tatu za kijeshi ziliharibiwa katika shambulio,” ilisema Al-Shabaab katika taarifa yake iliyohusisha picha zinazoonyesha ndege ikiwaka moto huku wapiganaji wake wakiwa wamesimama kando na ndege hiyo.
Kundi hilo la wapiganaji limedai kuhusika na shambulio hilo katika kaunti ya Lamu kwenye pwani ya Bahari ya Hindi nchini Kenya, eneo ambalo limekuwa kituo cha utalii kwa muda mrefu, lakini lililoko katika hatari ya vurugu za wanamgambo kutokana na ukaribu wake na Somalia.