×

MTOTO WA KAJALA GUMZO UBALOZI TAULO ZA KIKE

MTOTO wa staa wa Bongo Muvi, Kajala Masanja, Paula Paul, ameibua gumzo kama lote baada ya nyota yake kuonekana kuanza kung’aa mapema kutokana na kulamba dili nono la taulo za kike.  Gumzo lilianza kuibuka Ijumaa iliyopita muda mfupi baada ya kutangazwa na Kampuni ya Gerirwa ambayo inasambaza taulo za kike za Rani kuwa balozi kwa upande wa wanafunzi. Paula na mama yake waliingia mkataba wa kuzitangaza taulo hizo zinazotajwa kuwa na ubora wa hali ya juu kufuatia teknolojia yake mpya ya utengenezaji iitwayo Anion.

Muda mfupi baada ya Paula na mama yake kutangaziwa ubalozi huo katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Regency Park iliyopo Mikocheni jijini Dar, gumzo na maswali kutoka kwa wanahabari yalianza. Kutokana na hilo, gumzo kubwa lilizuka kila mmoja akimuelezea mtoto huyo kuwa muda si mrefu anaweza kuwa staa mkubwa.

“Nyota imeshaanza kung’aa kwa Paula na anaonekana anaweza kuwa staa mkubwa kama mama yake au hata pengine anaweza hata akamzidi. “Hebu kwanza muangalie anavyojiamini na kujielezea mbele ya wanahabari, yaani yuko vizuri mno,” alisikika mmoja wa waliokuwa wakishuhudia uzinduzi huo.

Baada ya kutangazwa kuwa balozi, Paula alijitokeza mbele ya wanahabari akionesha kujiamini na kuelezea furaha yake huku akitumia umombo (Kingereza) kuishukuru kampuni hiyo. Hata hivyo, wanahabari walimuomba azungumze Kiswahili kwa faida ya wasikilizaji wa Kibongo.

Paula alianza kuzungumza Kiswahili na kuelezea jinsi Kampuni ya Gerirwa itakavyorejesha furaha kwa wanafunzi wenzake nyakati za hedhi. Paula alisema mara kadhaa wanafunzi wa kike wamekuwa wakipata changamoto vipindi vya hedhi na kuwafanya washindwe kuhudhuria masomo, lakini aliishukuru Gerirwa kwa kuanzisha kampeni ya kuwasaidia bure wanafunzi wenye changamoto.

Hotuba fupi ya Paula ilizidi kuzua gumzo kwa jinsi alivyoelezea na kuonesha uelewa mpana. Akizungumza na wanahabari, mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hudaa Badi alisema sambamba na uzinduzi wa taulo hizo wamezindua kampeni ya kijamii iitwayo Rani na Binti Shuleni.

Rani na Binti Shuleni ni kampeni ambayo inalenga kusaidia wanafunzi wasioweza kuhudhuria shuleni wawapo katika hedhi kwa kuwapa taulo za kike. Shule zilizolengwa ni zile za sekondari ambazo zipo chini ya Serikali za mikoa yote hapa nchini, mpango huu unaenda sambamba na kampeni ya Serikali ya kutoa elimu bure ili mtoto wa kike asibaki nyuma.

Hudaa na mkurugenzi mwenza wa Gerirwa, Hawa Hassan walisema mwananchi yeyote anaweza kupendekeza shule yoyote ya sekondari ya Serikali ambayo anaona wanafunzi wake wana changamoto hiyo na wanahitaji msaada wa taulo hizo kutokana na hali yao kimaisha watume ujumbe kupitia namba 0754 311 616 au kupitia akaunti ya instagram #ranisanitarypad.

Akielezea sifa za taulo hizo, Hawa alisema zina kinga inayoua bakteria, wabaya na hazina muwasho, zinarekebisha vichocheo vya homoni na kusaidia kupunguza maumivu ya tumbo wakati wa hedhi. Pia alisema zina kinga zinazozuia hedhi kuvuja na kumuweka mtumiaji akiwa mkavu na salama ambapo pia husifika kwa kufyonza hedhi.

Alimalizia kwa kusema Pedi za Rani zinapatikana nchi nzima kwa bei ya jumla na rejareja kwa anayehitaji apige simu namba 0713311616 au 0754311616.

STORI: RICHARD BUKOS, DAR

Leave a Comment