
SULTANI Qaboos bin Said wa Oman aliyeitawala nchi hiyo kwa karibu nusu karne amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79, shirika la habari la taifa limeripoti.
Qaboos ambaye amekuwa sultani wa Oman tangu mwaka 1970 baada ya kumpindua baba yake, amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na inaaminika alikuwa akitibiwa saratani ya utumbo.
Kufuatia kifo chake, serikali imetangaza siku tatu za maombelezo ya taifa na bendera zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku 40.
Qaboos aliyepata elimu yake nchini Uingereza alifanya maguéuzi makubwa nchini Oman, taifa ambalo wakati akichukua madaraka lilikuwa na shule tatu pekee na sheria kandamizi zilizopiga marufuku nishati ya umeme, redio, miwani na hata matumizi ya miavuli.
Chini ya utawala wake, Oman ilikuja kufahamika kuwa eneo linalopendelewa zaidi na watalii na taifa kiungo kwenye eneo la Mashariki ya Kati likiisaidia Marekani kuwaokoa wanadiplomasia wake waliokamatwa mateka nchini Iran na Yemen na hata kuwakaribisha maafisa wa Israeli, wakati huohuo akipinga ukaliaji wa mabavu ardhi ya Wapalestina.
Kifo cha Qaboos kinatishia kuwepo wasiwasi wa kutokea machafuko kwenye taifa hilo la pembezoni ya Rasi ya Bara Arabu lenye raia milioni 4.6.
Sultani Qaboos ambaye hakuwa na mke wala watoto hakutaja hadharani mrithi wake.
Kulingana na katiba ya Oman familia ya sultani inapaswa kumtaja mrithi wa kiti hicho ndani muda wa siku tatu tangu kinapotangazwa kuwa wazi.
Iwapo familia itashindwa kuafikiana kuhusu jina la yule anakayechukua wadhifa huo, mtu aliyeteuliwa na Qaboos kupitia barua kwenda kwa familia yake ndiye atakuwa mrithi wa kiti cha usultani.
Katiba ya Oman inasema kuwa sultani anapaswa kuwa sehemu ya familia ya kifalme, muumini wa dini ya Kiislamu, mtu mzima, mwnye akili timamu na mtoto halali wa wazazi Waislamu wa Oman.
Nani anaweza kumrithi?
Wataalamu wa taratibu hizo wanasema kuna zaidi ya watu 80 wenye sifa za kumrithi sultani Qaboos.
Asad bin Tariq mwenye umri wa miaka 65 ndiye anatajwa zaidi kuwa jina lake ndiyo limo kwenye bahasha ya sultani baada ya kuteuliwa mwaka 2002 kuwa naibu waziri mkuu anayeshughulikia masuala ya kimataifa na mahusiano ya kigeni.
Barua hiyo ilikuwa ni ujumbe wa wazi kuwa marehemu Qaboos alikuwa akimuunga mkono binamu yake huyo.
Wengine wanaoweza kupewa nafasi hiyo ni binamu wawili wa Sultani Qaboos, Haitham bin Tariq, ambaye ni waziri wa utamaduni, na Shihab bin Tariq aliyekuwa mshauri wa karibu wa Qaboos.