
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesikitishwa na uamuzi wa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, wa kujiuzulu nafasi ya mnadhimu wa upinzani bungeni na kusema sababu alizotoa hazina mashiko.
Mbowe amesema ameshangazwa na taarifa ya Selasini kwamba hakuwahi kupewa barua ya uteuzi. Ameuliza iwapo hakupewa barua ya uteuzi imekuwaje aandike barua ya kujiuzulu?
Mbowe amesema Selasini ametumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili kwa uaminifu na anaheshimiwa na wabunge wote wa upinzani huku akipewa ushirikiano wote na Ofisi ya Bunge. Amekuwa akihudhuria vikao vyote vya kamati za uongozi na kulipwa posho.
Mbowe ameendelea kusema na kuuliza kama Selasini amefanya yote hayo ndani ya miaka miwili imekuwaje ashindwe kumalizia miezi minne iliyobaki kabla ya Bunge kuvunjwa?
Kiongozi huyo mkuu wa upinzani nchini ameonyesha wazi kutofurahishwa na uamuzi huo wa Selasini na kusema labda kama ana mambo yake ya siri ndiyo maana ameamua kufanya hivyo.
Mwezi uliopita katika uchaguzi mkuu ndani ya chama Selasini alikuwa anagombea nafasi ya Mwenyekiti Kanda ya Kaskazini lakini alipoteza nafasi hiyo kwa mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema.