
DAR: Ukisikia yeleuuwiii maana yake ni habari ya kushtua; kama hii ya mshereheshaji (MC) maarufu jijini Dar, Olivia Karumuna ‘MC Olivia’ kudaiwa kula rambirambi za Anna Zambi, Gazeti la IJUMAA linakupasha.
ANNA ZAMBI NI NANI?
Anna Zambi ni yule mtoto yatima aliyefiwa na wazazi pamoja na wadogo zake watatu mwishoni mwa mwaka jana katika ajali ya gari iliyotokea mkoani Tanga na msiba wake kuibua simanzi nzito ndani na nje ya Bongo.
UNDANI KUHUSU RAMBIRAMBI
Ilielezwa na chanzo chetu kuwa, kutokana na msiba mzito uliomfika binti huyo mwaka jana, kundi la mtandao wa WhatsApp lijulikanalo kwa jina la EKITOKE ambalo MC Olivia ni mwanachama wake, walikubaliana kuchangishana rambirambi kwa ajili ya kumfariji Anna.
“Kwa kweli lilikuwa wazo zuri, kila mmoja wetu aliliunga mkono kutokana na ukubwa wa msiba aliopata yule binti. “Viongozi wa kundi walimteua MC Olivia kuchangisha rambirambi hizo, kazi ambayo aliifanya na kukusanya kiasi cha shilingi laki tatu na elfu sabini na tano (375,000) kutoka kwa wanachama.
MC OLIVIA ADAIWA KULA RAMBIRAMBI
Chanzo kilidai kuwa, baada ya zoezi hilo kukamilika, wanachama walikubaliana kwamba fedha hizo ingawa ni chache waziwasilishe kwa mfiwa kama rambirambi yao.
“Wewe fikiria tangu mwezi wa 11 ulipotokea msiba hadi sasa fedha hizo hazijawasilishwa. Kila akiambiwa Olivia atoe fedha hizo apelekewe mfiwa, anaingilia huku, anatokea kule, fedha hazionekani! “Basi, baadhi ya wanachama wa EKITOKE wakaanza kumcharukia (MC Olivia) huku wakimtuhumu kuwa amekula fedha hizo za rambirambi alizotakiwa kupewa Anna kwa sababu alikuwa hataki kuzitoa,” kilidai chanzo chetu makini.
MC OLIVIA AMWAGA UTETEZI
Awali, mwandishi wetu alimtafuta MC Olivia ili ‘kubalansi’ tuhuma hizo nzito za kula rambirambi za mtoto yatima Anna ambaye hivi karibuni alifanikiwa kufaulu mtihani wake wa Kidato cha Nne kwa kupata ufaulu wa daraja la Pili, lakini simu yake ilionekana kuwa ‘bize’ muda mwingi ambapo alilazimika kumtumia ujumbe huu mfupi wa simu ‘SMS’.
“Olivia mimi ni Mhariri wa Global…kuna tuhuma zako kuwa umekula fedha za rambirambi za mtoto Anna Zambi aliyefiwa na wazazi wake…”
Baada ya dakika chache tangu ujumbe huo utumwe kwa MC Olivia, mshereheshaji huyo maarufu aliujibu kwa kuandika; “Habari…ndiyo, hizo tuhuma zipo ila siyo za kweli.” Wakati mwandishi wetu akijiandaa kumtumia ujumbe mwingine kumuuliza ukweli alio nao yeye ni upi? MC Olivia aliandika ujumbe mwingine uliosomeka hivi;
“Nipo safarini, nikirudi nitaweka kila kitu sawa.” Kwa mara nyingine mwandishi wetu alipotaka kujibu ujumbe huo kwa kumuuliza imekuwaje mpaka sasa hajaziwasilisha fedha hizo kwa mfiwa na akiwa yeye ndiye mkusanyaji ambaye alipewa jukumu la kumfikishia Anna fedha hizo, haraka MC Olivia alipiga simu na kukiri kukusanya rambirambi hizo.
“Mimi niko Arusha kwa sasa, nimekuja huku kwa ajili ya mambo yangu, narudi Ijumaa (leo) nafikiri, nikifika nitawapatia fedha hizo.”
Hata hivyo, MC Olivia alikana kula fedha za rambirambi huku akishangazwa pakubwa na tuhuma hizo ambazo aliahidi kuzimaliza kwa kuwashangaza wanaomtuhumu kula fedha hizo. “Nafanya mpango wa kutafuta hizo pesa na ikiwezekana hata kabla ya hiyo Ijumaa nitamtumia Admin (kiongozi wa kundi la WhatsApp la EKITOKE) na kumwambia jamani fedha zenu hizo.”
Hata hivyo, mazungumzo kati ya mwandishi na mtuhumiwa hayakutatua kitendawili cha “kwa nini mpaka leo fedha hizo hazijamfikia mfiwa?” Lakini MC Olivia mara kadhaa alisema kuwa, viongozi wa kundi wanajua kinachoendelea na kwamba aliamua kukaa kimya baada ya tuhuma za wanachama wenzake kuwa amekula fedha hizo kuwa nyingi.
Stori: Richard Manyota, Ijumaa