×

Sinema ya Kumuondoa Meya wa Dar, Hii Hapa

ILI kumuondoa madarakani Meya wa Jiji la Dar, Isaya Mwita, awali ilielezwa kuwa, kura moja zaidi ya mjumbe wa Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar ilihitajika.

 

Ni kwamba kuna mvutano mkali wa suala la Umeya wa Jiji la Dar kati ya CCM na Chadema. Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar walikutana wiki iliyopita huku wale wa CCM wakiitisha kura ya kutokuwa na imani na Meya Mwita anayetokea Chadema kufuatia ripoti ya kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda kuchunguza tuhuma dhidi ya meya huyo ya matumizi mabaya ya madaraka.

 

Hata hivyo, mkutano huo maalum ulimalizika kwa utata kutokana na kubainika kutotimia theluthi mbili ya wapiga kura ambayo ingeweza kumng’oa Mwita baada ya kukosekana kura moja.

 

Mvutano mkubwa ulizuka baada ya kugundulika kuwa jina la mjumbe mmoja, ambaye hakuwepo lilikuwa limeghushiwa na kujumuishwa kwenye orodha ya waliohudhuria mkutano huo na kuwafanya madiwani wa Chadema kucharuka kupinga.

 

“Leteni hilo daftari tulifute hilo jina,” ilisikika sauti ya mmoja wa wajumbe wa baraza hilo akisema kuonesha kwamba ni kweli jina hilo liliongezwa kimagumashi bila kujali kwamba hilo ni kosa la jinai. Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar lina wajumbe 26 kati yao CCM ni 16, Chadema saba na CUF watatu.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji kifungu cha 84 (1) kinaeleza ili uamuzi uweze kufanyika wa kumwondoa meya madarakani kutokana na sababu kadhaa, itapaswa kuwapo kwa theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri hiyo. Mtaalam mmoja wa hesabu aliliambia gazeti hili kuwa, theluthi mbili ya wajumbe 26 wa Halmashauri ya Jiji la Dar ni 17.

 

Kifungu hicho kinasomeka; “Halmashauri inaweza kumuondoa meya madarakani kwa kupata azimio linaloungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri kutokana na hoja au sababu yoyote. Mojawapo ni kutumia vibaya ofisi yake.”

 

Hii ina maana kuwa ili Meya Mwita aweze kung’olewa kwa mujibu wa kifungu hicho cha 84 (1), CCM walipaswa kupata kura moja kati ya 10 za wajumbe wa upinzani.

Hata hivyo, katika mkutano huo ilishindikana kupata theluthi mbili kwani kura zilizopigwa zilikuwa 16. Lakini ameng’olewa!

 

Uchunguzi wetu umegundua kutotimia theluthi mbili ya kura kulichangiwa na kukosekana kwa Diwani wa Minazi Mirefu, Kassim Mshamu kutoka CUF. Hata hivyo, jina la Mshamu lilikuwemo kwenye orodha ya wajumbe waliohudhuria kikao na kuzua mtafaruku baada ya wajumbe wa Chadema kudai jina lake lilikuwa limeingizwa kwa kughushi.

 

Kimsingi ilikuwa kama Mshamu ndiyo aliushikilia umeya wa Mwita kwani kura yake ilikuwa ni turufu ya Chadema na CCM na kutotokea kwake ndiko kuliongeza mvutano wa pande mbili hizo.

Awali katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Jiji, Sipora Liana alidai Mwita anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo kutotumia shilingi bilioni 5.8 za Shirika la Usafiri Dar (Uda).

 

Fedha hizo zilitolewa na Kampuni ya Simon Group kwa ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda. Liana aliwasilisha taarifa hiyo huku akiwataka wajumbe wa CCM na Chadema waliokuwemo kwenye kikao hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani na Mwita kwa mujibu wa kanuni, akisema kamati iliyomchunguza ilipendekeza jiji kufuata miongozo na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yake na ukiukwaji wowote utachukuliwa hatua stahiki.

 

Mchakato wa upigaji kura ulifanyika kwa mtindo wa wajumbe wa CCM 16 kusimama kuashiria kutokuwa na imani na Mwita, wakati wale wa Chadema walikaa kuashiria kupinga hoja hiyo.

 

Baada ya hatua hiyo kukamilika, Naibu Meya wa jiji hilo; Abdallah Mtinika aliyekuwa akiongoza kikao hicho alitangaza matokeo kwa kusema; “Kura zilizopigwa ni 16, mjumbe mmoja ameomba udhuru na wawili hawakupiga kura, uamuzi wenu umepitishwa na kikao kimefungwa,” ikidhaniwa kuwa sinema ingeishia hapo.

 

Badala yake, hatua hiyo ilizua mtafaruku mkubwa baada ya wajumbe wa Chadema waliokuwa wanne katika kikao hicho wakiongozwa na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kusema bado wanamtambua Mwita kuwa Meya wa Jiji kwa kuwa mkutano huo haukutimiza akidi inayotakiwa kumuondoa.

 

Mtinika alikaririwa akisema kuwa yeye ndiye naibu meya wa jiji hilo baada ya wajumbe wa CCM kuazimia kutokuwa na imani na meya aliyekuwa madarakani.

“Hatujamtoa Mwita kwenye udiwani, bali nafasi ya umeya, lakini ana uwezo wa kukataa rufaa kwa Waziri wa Tamisemi (Seleman Jafo),” alisema Mtinika.

 

Mkanganyiko zaidi umeibuka baada ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar, Liana kudai kuwa wajumbe 16 ambao walipiga kura ya kutokuwa na imani na meya, walifikisha theluthi mbili huku wajuzi wa hesabu wakisema ilitakiwa wawe 17.

 

Meya Mwita baada ya mkutano huo, Jumatatu iliyopita alifika ofisini kwake katika Jengo la Karimjee ili aendelee na majukumu yake ya kila siku, lakini akashindwa kuingia baada ya nywila (password) ya mlango wake kubadilishwa.

Lakini Mkurugenzi wa Jiji la Dar, Spora Liana alisema tayari wamempa barua ya kumng’oa kwenye nafasi yake Meya Mwita.

 

Mkurugenzi Liana alipoulizwa na safu hii kuhusu madai ya kughushi jina la mjumbe wa CUF alisema mwenye malalamiko aende Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru). Tungoje sinema hii sehemu ya pili!

Na Elvan Stambuli

Simu: 0655-339616

Leave a Comment