
ALIYEKUWA mbunge wa Kilombero (CHADEMA) kisha kuhami CCM, Peter Lijualikali, amefunguka kuwa cheo cha urais wa Tanzania si pole kwa mgonjwa wala si huruma bali ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii na kuwa mzalendo kwa nchi yako.
Lijualikali ametuma ujumbe huo kupitia ukurasa wake wa Twitter na huku akichapisha na picha ya kuonyesha kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwenye kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mapema mwezi Oktoba.
“Urais wa Nchi ya Tanzania sio Pole kwa Mgonjwa. Urais wa Nchi yetu sio huruma. Urais wa Nchi yetu ni matokeo ya uchapakazi, uwajibikaji, uzalendo na uadilifu kwa Taifa letu. Ni Magufuli Tena 2020-2025!, Viva CCM, Viva Magufuli, Hapa Kazi Tu” amendika Lijualikali.
Lijualikali alitangaza kukihama chama chake cha CHADEMA na kujiunga na CCM siku chache kabla ya kumalizika kwa vikao vya bunge la 11 jijini Dodoma na hakufanikiwa kuchaguliwa kwenye mchakato wa awali wa chama hicho wa mgombea ubunge kwenye jimbo la Kilombero.