
BAADA ya beki wa Yanga, Ally Mtoni ‘Sonso’ kupata kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Azam ambao walipoteza kwa bao 1-0, beki huyo amewaomba radhi mashabiki, viongozi na wanachama wa timu hiyo.
Sonso alipewa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga beki wa Azam, Nicholaus Wadada, ambaye pia alimchezea rafu mbaya Sonso ambayo mwamuzi hakuiona jambo lililosababisha Sonso kumkanyaga ambapo mwamuzi alimuona na kumpatia kadi hiyo nyekundu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Sonso alisema kuwa alifanya makosa ambayo hatayarudia tena, hivyo anawaomba msamaha mashabiki wa Yanga, viongozi wa mpira wa pande zote kwa yaliyotokea.
“Kwenye mpira kuna mengi sana ambayo huwa yanatokea, yale yalishapita, kikubwa kwangu nawaomba msamaha mashabiki na wapenzi na viongozi wa Yanga, bila kuwasahau viongozi wote wa mpira hapa nchini kwa kilichotokea, naamini sitakifanya tena,” alisema beki huyo.
Yanga chini ya kocha mpya Luc Eymael katika michezo miwili aliyoiongoza timu hiyo imepata kadi nyekundu mbili moja dhidi ya Kagera Sugar, aliyopewa kiungo Mohamed Banka ambapo Yanga walipoteza kwa mabao 3-0, ya pili ni ya Ally Mtoni Sonso dhidi ya Azam waliyopoteza kwa bao 1-0.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam