×

Prof. Kabudi: Niliandika Barua kwa Rais Kujiuzulu – Video

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema kuwa ilifika wakati akakata tamaa kuhusu ugumu wa makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Madini ya Barrick na kuamua kuandika barua ya kujiuzulu uwaziri.

 

Kabudi amesema hayo wakati akihutubia kabla ya utiaji saini makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kampuni ya  Barrick leo Ijumaa, Januari 24, 2020, asubuhi Ikulu, Dar es Salaam.

 

“Mheshimiwa rais uliponipa jukumu hili nilijiuliza kwa nini amenipa kazi hii ni ngumu ya lawama, ya kubezwa,  ya kupuuzwa?

 

“Hawakuwa hawa, walikuwa wenzao ambao hawapo,  sipendi kutaja majina, walikuwa hawataki mikataba isainiwe, wenzangu wanafahamu. Ilifika mahali nilitaka kuingia dhambi ya kukata tamaa kwamba kazi uliyonipa imenishinda. 

 

“Mheshimiwa rais hili nalisema japo wenzangu walinisii nisiliseme. Mheshimiwa rais nilikuwa nimeandika barua ya kujiuzulu kwamba kazi uliyonipa imenishinda, aibu hii na fedhea hii nitaibeba, barua sikuileta kwa sababu Kasmilius alininyang’anya na kuichana.

 

“Wakati wa majadiliano kati ya Tanzania na Barrick, Prof. John Thornton alikubali mikataba haikuwa mizuri na lazima irekebishwe, na Rais Magufuli alisema sitaki mikataba irekebishwe kwa ajili yangu, fedha yote itakayopatikana itakwenda kwenye shule, afya, miundombinu n.k.

 

”Kazi uliyotupa tumeifanya kwa akili zetu zote, kwa nguvu zetu zote na uwezo wetu wote na niombe msamaha kwako na kwa Watanzania wote kwa lolote litakalokuwa limepungua limetokana na ubinadamu wetu labda upeo wetu…” amesema Prof. Kabudi.

 

Vilevile, akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mark Bristow, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold, miongoni mwa mambo mengine, alisema: “Watu wengine walikosoa msimamo wako (Rais John Magufuli) kwamba unafukuza wawekezaji lakini tumefikia mahali ambapo kama tunapata, tunapata wote na kama tunakosa, tunakosa wote.” 

TAZAMA VIDEO YA TUKIO

Leave a Comment