
TIMU ya Simba Sc jana Jumatano, Januari 29, 2020, imeibuka na ushindi wa bao 3-2 dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kocha wa Namungo, Hitimana Thiery amesema; “Wachezaji na benchi la ufundi hatukuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya mchezo kuanza kwa sababu kulikuwa na harufu ambayo haikuwa rafiki kwetu kukaa humo. Tulikaa nje ya vyumba, siwezi kujua ni harufu ya nini…….. Tulikuja kutafuta matokeo lakini itabidi tuangalie TV vizuri nafikiri goli la tatu ilikuwa off-side,” amesema Kocha Thiery.
Simba walianza kupata bao kupitia kwa Francis Kahata dakika ya 22 lililosawazishwa na Bigirimana Blaise dakika ya 36 huku Hassan Dilunga akafunga bao la pili akiwa nje ya 18 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango Balora dakika ya 39 na kuwafanya Simba kuenda mapumziko wakiongoza kwa mabao 2 -1.
Kipindi cha pili Namungo walipata bao la pili kupitia kwa Lucas Kikoti dakika ya 72 ambaye aliachia shuti kali akiwa nje ya 18 alichoambulia Kakolanya ilikuwa kuokota mpira nyavuni.
Dakika ya 89, Kagere alimaliza shughuli uwanjani kwa kufunga bao la ushindi ambalo limewapa Simba pointi tatu jumla. Simba sasa inafikisha jumla ya pointi 44 ikiwa nafasi ya kwanza na imefunga jumla ya mabao 38.