
Msanii wa muziki Bongo, Vanessa Mdee ‘V Money’ amelamba shavu la ubalozi katika kampuni ya KEDS TANZANIA COMPANY ambayo inatengeneza sabuni ya unga ya Doffi. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutiliana saini na kampuni hiyo, Vanessa amesema amefurahi kupewa ubalozi huo kwa kuwa na yeye ni msanii ambaye ana program ya kusaidia jamii.
“Nimefurahi kwa sababu wameniona ninafanya vitu vingi vizuri kwa jamii na hata mwaka jana tulianza na viatu vya shule mwaka huu nimechaguliwa kuwa balozi wa sabuni ya Doffi ambayo ni nzuri kwa kinadada na wakinamama ambao ndiyo wadau wakubwa wa suala kufua, kuoshea vyombo na vitu vingine” Alisema.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Ben Song alisema kuwa wameamua kumpa Vanessa ubalozi huo kwa sababu ni msanii ambaye anafanya vizuri kimuziki Afrika nzima kwa hiyo wanaamini kuwa ataweza kuitangaza vyema sabuni ya Doffi.
“Tumechagua Vanessa kwa sababu ni msanii mkubwa Afrika na bidhaa yetu ni nzuri na inapatikana ikiwa na harufu ya limau na maua kwa ajili ya matumizi ya usafi.”Alisema.

Vanessa akiwa na viongozi wa kampuni hiyo.
HABARI: NEEMA ADRIAN
PICHA: RICHARD BUKOS GPL
