×

Chagueni Moja; Kumtumikia Mungu au Wanadamu

KATIKA siku tulizonazo, Dunia imebadilika. Watu wanamuona Mungu wa kawaida. Dhambi zinazidi kuwa nyingi kadiri siku zinavyosonga. Wanandoa wanauana. Mapenzi ya jinsi moja yameshamiri. Baadhi ya watumishi wa Mungu wamegeuka matapeli.

 

Nini maana yake? Hizi ni dalili za siku za mwisho. Hatuna budi kumrudia na kumtumikia Mungu kwa mioyo yetu yote. Wapo baadhi waliogeuza dini kuwa kitu cha utani. Kila mtu anafanya atakavyo.

 

Kwenye ulimwengu wa wasanii wa muziki, hivi karibuni kumeibuka baadhi yao wanaofanya Bongo Fleva ambao wamesikika wakiimba Injili. Wapo wengine ni waimbaji wa Injili, lakini matendo yao hayaendani na utumishi wao kwa Mungu, hivyo wanapaswa kuchagua moja; ama kumtumikia Mungu au kuwatumikia wanadamu.

NANDY

FAUSTINA Charles Mfinanga ‘Nandy’ ni miongoni mwa wanamuziki wakali wa Bongo Fleva ambaye amekuwa akiimba nyimbo za kidunia, lakini pia akifanya covers (kurudia nyimbo) za nyimbo za Injili za waimbaji mbalimbali.

Miongoni mwa covers hizo ni Nikumbushe wa Angel Bernad na Mimi ni wa Juu wa Joel Lwaga.

 

KUHUSU NANDY

“Kama anazitumia hizo covers kibiashara ni sawa, lakini hakuna mtu anaweza kumkaribisha kuimba huo Wimbo wa Angel Bernad au Joel Lwaga kwenye madhabahu yoyote. Labda mpaka aamue kutoka kabisa huko aliko na ahamie kwenye Gospel. Nandy ni binti mzuri ambaye anapenda sana nyimbo za Injili, hivyo ninamshauri kama anampenda Mungu na anajisikia kuimba nyimbo za Gospel, basi akate shauri ili aimbe nyimbo za Gospel.”

GOZBERT

HUYU alifahamika zaidi kwenye nyimbo za Injili. Amekuwa akishika akili za mashabiki wake kwa kuimba nyimbo nzuri na zenye ujumbe mzito. Ni msanii ambaye mara kadhaa amekuwa akinukuliwa akisema kuwa huwa anawaandikia mashairi wasanii wa Bongo Fleva. Pia amekuwa akishiriki kwenye matamasha ya kidunia kiasi cha kuibua mjadala kila kona.

 

Moja ya maswali ambayo watu wengi wamekuwa wakijiuliza… je, ni sahihi kwa msanii kuimba nyimbo za Injili na zile za kidunia kwa wakati mmoja? Majibu yake ni kwamba, haoni kama kuna tatizo!

 

KUHUSU GOZBERT

“Kuhusu Gozbert kupafomu kwenye jukwaa la wanamuziki wa kidunia, sidhani kama ni tatizo kwa sababu ile sehemu watu wamechanganyikana. Kuna wengine ni Wakristo na nyimbo nyingi alizoimba ni za Injili, alishuhudia watu kwa sababu kuna watu wengine wanapenda nyimbo za Injili. Hivyo nina imani kuna ambao aliwagusa kwa namna moja au nyingine.”

BEN POL

BENARD Paul ‘Ben Pol’ ni mwanamuziki mzuri wa Bongo Fleva, lakini hivi karibuni aliachia wimbo wa Injili unaokwenda kwa jina la Ebenezer.

Alipohojiwa na Gazeti la IJUMAA juu ya wimbo huo, Ben Pol alisema; “Lengo ni kuonesha utofauti. Nimetoa wimbo huu na nitaendelea kutoa nyingine nyingi za tofauti.”

 

KUHUSU BEN POL

Stella: “Ben Pol anatakiwa aamue moja, akiamua kuwa upande wa Gospel (Injili) awe Gospel na akiamua kuimba Bongo Fleva, basi abaki hukohuko. Hii ni kwa sababu hivi ni vitu viwili tofauti. Huwezi kuwatumikia mabwana wawili. Kwa upande wa masuala ya kiroho, tunaangalia sana, tunaposema Gospel maana yake ni Injili inayoleta wokovu.

 

“Huwezi kusimama madhabahuni, halafu ukawa na vitu viwili, yaani ukamuwakilisha Mungu na shetani. Haitakubalika.”

EMMANUEL MBASHA

NI baba mlezi na mshauri wa wasanii wa nyimbo za Injili Bongo, lakini mara kadhaa amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kujibizana na baadhi ya mashabiki wake kisha kujikuta akitoa lugha mbaya. Hali hii imekuwa ikiibua minong’ono kuwa, inakuwaje mtumishi wa Mungu anakuwa na matendo sawa na watu wa kidunia? Hivi karibuni ilivuja video ya Mbasha ikimuonesha akiwa jukwaani akipafomu nyimbo za Injili huku akikata mauno ya hatari, jambo lililowafanya baadhi ya mashabiki kuhoji kulikoni?

 

Katika mkanganyiko kama huu, Gazeti la IJUMAA lilitaka kujua usahihi ni upi ambapo lilifanya mahojiano na Katibu wa Chama cha Muziki wa Injili Tanzania (Chamuita), Stella Joel ambaye anafunguka kama ifuatavyo;

 

KUHUSU MBASHA

“Japokuwa hiyo video sijaiona, lakini kama alikuwa anaimba Injili na alikuwa amevaa mavazi ya kujisitiri, sioni kama kuna tatizo, ingawa ninawashauri wanamuziki wa Injili wacheze vizuri, wasitumie mitindo ambayo inaashiria ngono, maana kukata viuno kupita kiasi ni mambo ambayo yanachochea uzinzi. Pia kuhusu hiyo tabia yake ya kujibizana na mashabiki vibaya mitandaoni siyo sawa kwa sababu hilo siyo tu halikubaliki kwa Mungu, bali pia ni kosa kisheria.”

 

USHAURI: Kama mwanamuziki, hutakiwi kuwa uvuguvugu (yaani leo unakuwa moto kesho baridi). Unatakiwa uamue jambo moja, kumtumikia Mungu au wanadamu ili mwisho wa siku hata mashabiki wawe wanajua wewe upo upande upi.

MAKALA: Memorise Richard

Leave a Comment