×

Masau Afunguka Alivyochukuliwa na Polisi Dar

MSEMAJI wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amefunguka kuhusu tukio la kutolewa kwake na polisi uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Yanga ulioisha kwa Ruvu kupoteza kwa bao 1-0.

 

Masau baada ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Uhuru Jumamosi iliyopita, hakuweza kuondoka na wenzake kutokana na kupewa tahadhari na wana usalama kufuatia mashabiki wa Yanga kumtafuta wakimzomea na hivyo kuzua taharuki.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Masau alisema kuwa kilichowafanya mashabiki wengi wa Yanga kumtafuta ni kwa sababu walikuja uwanjani na hofu ya kupoteza mchezo huo kutokana na ubora wa Ruvu na ushindi walioupata ilikuwa kama ‘sapraizi’, hivyo wakataka kumjibu.

 

“Sikuweza kuondoka na wenzangu baada ya mchezo kuisha kutokana na kuzuiliwa na wana usalama kwani kuna baadhi ya mashabiki walionekana kunipania na ikabidi baada ya muda wanitoe uwanjani kwa usaidizi wa polisi.

 

“Hii ni kwa sababu mashabiki hao walikuja uwanjani wakiwa na hofu ya kupoteza mchezo huo kwani wanajua fika ubora tulionao ndio maana baada ya kushinda hawakuonekana kuamini na ndipo walianza kunitafuta,” alisema Masau.

JOEL THOMAS, Dar es Salaam

Leave a Comment