KOCHA wa Yanga Luc Eymael amesema kuwa atafanya mabadiliko ya kikosi chake katika mchezo wa leo Jumanne pindi watakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya Mbeya City.
Eymael amepanga kuwatumia Kelvin Yondani, Tariq Seif, Feisal Salum na Mrisho Ngassa katika mchezo huo, baada ya timu yake kucheza michezo zaidi ya minne ikiwa haina mabadiliko makubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Eymael alisema imefika wakati sasa wa kutoa nafasi kwa wachezaji wengine kutoa nguvu zao katika timu hiyo, kwani kuna baadhi ya wachezaji wamecheza mechi nyingi mfululizo hivyo wanatakiwa kupumzika na kuwapa nafasi wenzao kuweza kucheza, huku akiongeza kuwa mabadiliko hayo hayataleta athari kwa kuwa wachezaji wote wapo vizuri na morali ya hali ya juu.
“Nashukuru Mungu kuwa timu imepata matokeo katika michezo yote ya hivi karibuni na kuna wachezaji wamecheza mechi nyingi bila kupumzika, nafikiri imefika wakati sasa wa kutoa nafasi kwa wachezaji wengine na wao watoe mchango wao.
“Tariq alitakiwa kucheza dhidi ya Ruvu Shooting lakini nikaona muda hautoshi, Ngassa, Yondani wote wapo vizuri nafikiri watatakiwa kucheza katika mechi zijazo ikiwemo na hiyo ya Jumanne,” alisema Luc.
