RAIS John Magufuli amewataka wananchi wote wote wanaojenga kwenye mabonde waache na waondoke wenyewe, wayaachie maji yapite na mabonde yatumike kwa ajili ya kulisha mifugo na kulima lakini si kwa ajili ya makazi.
Magufuli amefanya uamuzi huo leo Jumanne, Februari 11, 2020, eneo la Gezaulole, Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es salaam wakati akihutubia baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni na Jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.
“Inawezekana mwaka huu ukawa mbaya kwa sababu watu tumekalia kulalamika mafuriko na hatulimi baadaye maji yatakapopotea tutaanza kulalamika njaa na Mungu atatushangaa alituletea maji hatukuyatumia halafu atuletee jua ambalo halina mafuriko tuanze kulalamika njaa.
“Wakiwa na mafuriko huko, wewe unalima kunde. Wakiwa na mafuriko huko, wewe unafanya kazi ili baadaye watakapotoka wa kwenye mafuriko waje kula chakula chako kwa kuwatwanga pesa. Huo ndiyo ukweli ndugu zangu lazima niwaeleze.
“Kuna ndugu zangu Wasukuma wameenda Lindi kule wakaenda na ng’ombe zao wakakaa kwenye mabonde, maji yamekuja yamewachukua. Watani zao wa lindi walikaa mlimani, Msukuma alipoona majani mazuri ya baridi, maji yalipokuja yamepeleka na baadhi ya ng’ombe wao. Hakuna cha kusaidiwa uliyatafuta mwenyewe hayo mabonde, ngoja yakuondoe ili ujifunze vizuri,” amesema Rais Magufuli.
“Nilifuta hati ya umiliki wa eneo hili iwe chini ya Serikali lakini nimeambiwa umiliki haujarudishwa kwenye Manispaa, najua kuna Mawaziri hapa kamuelezeni Waziri mwenzenu wa ardhi ndani ya wiki moja umiliki wa ardhi hii uwe chini ya Manispaa ya Kigamboni”
“Nitoe wito kwa Viongozi wa Kigamboni, ukubwa wa eneo hili ni Ekari 750, isije kutokea baada ya kurudishiwa mkaanza kugawana nyinyi, hapo ndio mtajua kama mpo Kigamboni, Kisarawe au Mkuranga, itunzeni hii ardhi sio ya Viongozi ni ya wakazi wa Kigamboni.
“Nafahamu mlikuwa na matatizo na Afisa Ardhi wa Kigamboni ni mtoro hajafanya kazi karibu miezi mitatu na aliandikiwa barua lakini Wizara ya Ardhi bado wanaleta mshahara wake, shughulikieni Watendaji ambao wanawachelewesha.
“Nataka ndani ya wiki hii Wafanyakazi hasa Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wahamie Kigamboni ili iwe rahisi kutoa huduma kwa Wananchi, zile nyumba zilizotolewa na NSSF ni nyumba za Serikali hivyo wafanyakazi hawa wakae bure kwa mwaka mmoja”- Rais JPM.
“Natoa agizo kwa TAMISEMI kutafuta Tsh. Billion mbili kwa ajili ya kujenga nyumba za Watumishi wa Wilaya ya Kigamboni ili baada ya muda watoke kwenye nyumba za NSSF na kuhamia kwenye nyumba zao, na Mkandarasi ajenge nyumba hizo kwa miezi 6 na msiweke 10%,” amesema Rais Magufuli.

