BADAA ya Ditram Nchimbi kutoa pasi mbili za mabao katika michezo miwili mfululizo akitokea pembeni, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, ameonekana kunogewa zaidi kumpanga mchezaji huyo pembeni tofauti na nafasi yake iliyozoeleka.
Nchimbi akiwa na Polisi Tanzania alikuwa akitumika kama mshambuliaji wa kati lakini chini ya kocha Eymael amemchezesha pembeni katika michezo miwili mfululizo dhidi ya Lipuli na JKT Ruvu ambapo amefanikiwa kutoa pasi mbili za mabao huku zote akimpatia Molinga.
Eymael ameliambia Championi Jumatatu kuwa ataendelea kumtumia mshambuliaji huyu pembeni kwani ameonyesha kupaweza zaidi kutokana na mchango wake mzuri aliouonyesha akitokea pembeni tofauti na katikati.
“Nchimbi ni mchezaji mzuri sana, anacheza kwa kufuata maelekezo yangu ipasavyo, napenda sana akicheza katikati lakini kwa kuwa pembeni pia anacheza vizuri, basi nitamtumia pembeni kutokana na uwezo aliouonyesha.
“Tayari ameshatuonyesha mchango wake akiwa pembeni tofauti na alipocheza akiwa mshambuliaji wa kati, nafurahia kuwa katika kikosi changu kwa kuwa ni mchezaji mzuri na atatusaidia,” alisema kocha huyo.
MARCO MZUMBE, Dar es Salaam
