×

Mtuhumiwa Wizi wa Watoto Kupimwa Akili

MBEYA: Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mbeya, imeagiza kwenda kupimwa afya ya akili kwa mkazi wa Tegeta jijini Dar anayetuhumiwa kwa wizi wa watoto wawili mwishoni mwa mwaka jana jijini Mbeya.

 

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Davice Msanga kuiomba mahakama kwenda kupima afya ya akili ya mshtakiwa huyo, Hawa Ally (40) aliyedaiwa kutenda kosa hilo Desemba 28, mwaka jana katika eneo la Ituha jijini Mbeya.

 

Februari 6, mwaka huu, mtuhumiwa huyo alifikishwa mbele ya mahakama hiyo na aliposomewa shauri hilo alikana makosa yote mawili na kusema watoto hao alipewa na kunguru na kuamua kuondoka nao.

 

Jambo la kushangaza ni baada ya kushuhudia mtuhumiwa huyo ndani ya kipindi cha wiki moja na siku sita akiwa gerezani akisema mwanamke mmoja ambaye hakumtaja jina alimpelekea mtoto mwingine mkubwa na hajaeleza mtoto huyo aliko.

Maelezo hayo yaliufanya upande wa mashtaka kuiomba mahakama mtu huyo kupimwa afya yake ya akili ili kuendelea na hatua inayofuata na mahakama imekubali ombi hilo.

 

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, siku ya tukio mshtakiwa, baada ya kuiba watoto hao jijini Mbeya alisafiri nao hadi mkoani Tabora ambapo alimwacha mmoja Tabora Mjini baada ya kumkataa na kuendelea na safari na mwingine ambaye naye alianza kuumwa hatua, iliyomfanya atafute hospitali ili kwenda kumtibu ndipo alikamatwa baada ya kutiliwa shaka.

 

Kosa hilo ni kinyume na kifungu namba 169 (1) a cha sheria ya kanuni ya adhabu hivyo baada ya uchunguzi huo kukamilika Jamuhuri itaita mashahidi ili kuthibitisha mshtakiwa Hawa kutenda kosa hilo la wizi wa watoto ambao baada ya kupatikana walikabidhiwa kwa wazazi wao katika uwanja wa FFU Mbeya.

 

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mbeya, Zawadi Laizer aliahirisha shauri hilo na kuruhusu mshtakiwa Hawa kwenda kupimwa akili huko Mirembe mkoani Dodoma hadi Machi 19, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa wakati taratibu za kumsafirisha zikifanyika kutokana na kwamba hajapata dhamana mpaka sasa.

Stori: Ezekiel Kamanga, Wikienda

Leave a Comment