
BAHATI nasibu ya Chomoka na Gari Mpya iliyoanzishwa na Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti yake ya michezo ya Championi na Spoti Xtra, imeendelea kushika kasi katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar.

Timu ya masoko ya Global Publishers, Februari 27, 2020, ilizunguka katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo kuitangaza bahati nasibu hiyo, ambapo waligawa zawadi mbalimbali kwa wasomaji wa Championi na Spoti Xtra.
Baadhi ya maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambayo Timu ya Promosheni ya Baba Lao ilitia timu ni pamoja na Bamaga, Mwenge Stand, Mawasiliano, Mabibo Sokoni, Kigogo Ruhanga, Magomeni Mikumi, Popo Bawa Tandale, Friends Corners, Sinza Kijiweni naSinza Mori.

Uzinduzi rasmi wa bahati nasibu hiyo ulifanyika jana Alhamisi katika Ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza Mori jijini Dar, ambapo Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani alikuwa mgeni rasmi akimuwakilisha Rais wa TFF, Wallace Karia.

Bahati nasibu hiyo inatarajiwa kudumu kwa takribani miezi mitatu na mshindi wa jumla atajinyakulia gari mpya aina ya Toyota Funcargo huku wengine wakizoa simu mpya na zawadi nyingine kibao kila wiki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Nyamlani alianza kwa kuyapongeza magazeti ya Championi na Spoti Xtra kwa kuandika habari za ukweli na za uhakika huku akichagiza kwamba yeye ni msomaji mkubwa wa magazeti hayo, huku akiwataka wasomaji wengine kutumia fursa hiyo kujishindia zawadi hizo.

Nyamlani aliongeza kuwa, ni jambo zuri sana kuona magazeti hayo yanakumbuka wasomaji wake na kurudisha kwa jamii, kwani kuandaa bahati nasibu hiyo ni zaidi ya kutambua mchango wa wananchi ambao siku zote wamekuwa wakisoma magazeti hayo na kupata taarifa mbalimbali za kimichezo.

Mbali na hilo, Nyamlani alipongeza juhudi za waandishi wa Gazeti la Championi na Spoti Xtra, kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa weledi mkubwa bila kumgandamiza yeyote jambo ambalo limekuwa msaada katika harakati za kukuza michezo hapa nchini.

“Mimi ni msomaji mzuri sana wa magazeti haya, ni magazeti mazuri sana ambayo huwa yanaandika habari za ukweli na uhakika jambo ambalo ni msaada katika maendeleo ya soka letu na michezo kwa jumla, hivyo niwapongeze waandishi na uongozi kwa kuwa wamekuwa wakishirikiana na sisi TFF.

“Kuhusu bahati nasibu, niwapongeze, naamini mnarudisha shukrani zenu kwa jamii ambayo siku zote imekuwa ikiwasapoti katika habari ambazo mnaziandika na wao wananunua magazeti na kuzisoma,” alisema Nyamlani.

Naye Meneja wa Global Publishers, Abdallah Mrisho, alisema: “Tunahitaji wasomaji wetu waweze kujikwamua kiuchumi ndiyo maana tumetoa zawadi ya gari ambalo naamini kama mshindi atashinda gari hili ataweza kulitumia kama taksi ama usafiri wake binafsi, hivyo watu wanunue zaidi Gazeti la Championi na Spoti Xtra waweze kujishindia.

“Gazeti la Spoti Xtra ambalo linatoka kila Alhamisi na Jumapili, linauzwa Sh 500 na Championi linalotoka Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumamosi linapatikana kwa Sh 800 tu.”

Kwa upande wa Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally, alisema: “Championi na Spoti Xtra ndiyo magazeti bora ambayo yana habari bora zilizojaa takwimu za uhakika hapa nchini, hakuna gazeti ambalo utapata kila kitu isipokuwa Championi na Spoti Xtra.

“Lakini pia katika kila shindano au promosheni inayoletwa na magazeti haya, hutoa zawadi za ukweli kabisa tofauti na watu wengine ambao hudanganya, hivyo wasomaji kupitia magazeti haya washiriki na waone jinsi gani watakavyoshinda zawadi kemkem.”
Mtangazaji wa +255 Global Radio, Gaby Mtanzania, ambaye aliambatana na timu ya masoko kwenda mtaani kuinadi bahati nasibu hiyo, alisema kuwa: “Muitikio umekuwa mkubwa sana, tulipita katika mitaa mingi kama Mwenge, Manzese, Ubungo, Magomeni, Sinza na maeneo mengine ambapo mbali na kuionyesha gari mpya itakayogambaniwa pamoja na simu, lakini wananchi waliweza kupata zawadi za tisheti bure kabisa.”

JINSI YA KUSHIRIKI
Nunua Gazeti la Championi au Spoti Xtra, kisha fungua ukurasa wa pili ambapo utakutana na kuponi yenye maelekezo ya kushiriki bahati nasibu hiyo. Jaza kuponi kama maelekezo yalivyo.

JINSI YA KUTUMA
Mpe kuponi yako muuza magazeti aliye karibu nawe popote ulipo, au peleka kwenye Ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza Mori, Dar, au tuma kwa njia ya barua, Jishindie Gari, Global Publishers, S.L.P 7534, Dar es Salaam.
Kwa maelezo zaidi, piga simu no: 0717 020792 au 0672 324759.

MASHARTI YA KUSHIRIKI
Wafanyakazi wa Kampuni ya Global Publishers & General Enterprises Ltd na watoto chini ya miaka 18 hawaruhusiwi kushiriki bahati nasibu hii.
Kuponi zitumwe kutoka nakala halisi ya gazeti, vivuli (fotokopi) haviruhusiwi. Mtu anaruhusiwa kutuma kuponi nyingi kadiri awezavyo ili ajiongezee nafasi ya kushinda.
Kuponi zote zitachezeshwa kwenye droo ya awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu.
Na Mwandishi Wetu
