KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, amefikisha ujumbe mzito kwa wapinzani wake Simba kuwa watakapokutana wasitarajie wepesi hata kidogo kutoka kwao.
Kocha huyo ameongeza kuwa Simba wasitarajie kwamba watapata ushindi kwao kirahisi kwa sababu michezo ya dabi haijawahi kuwa rahisi sehemu yoyote itakapochezwa.
Eymael, raia wa Ubelgiji, amesema hayo ikiwa Jumapili hii Yanga watakuwa wenyeji wa Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo itapigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa na upinzani kutokana na matokeo ya sare ya mabao 2-2 waliyoyapata timu hizo katika mechi ya kwanza Januari 4, mwaka huu.
Eymael ameliambia Championi Jumatatu, kuwa siku ambayo watacheza na Simba watacheza vizuri zaidi kwa kuelewa kuwa wapinzani wao ni timu ambayo ina uwezo mkubwa.
“Tutacheza vizuri mbele ya Simba tutakapokutana nao, kwa sababu wao ni wapinzani wa tofauti ambao wana uwezo mkubwa katika ligi.
“Lakini haitakuwa rahisi kwao kuweza kushinda katika mechi hii kwa sababu derby siku zote siyo mechi ya kirahisi, ina matokeo yake mengine tofauti na wao ambavyo wamekuwa wakiwaza kwamba watapata ushindi kilaini,” alisema Eymael.
Said Ally, Dar es Salaam
