×

Luis Ameshindikana, Hivi Ndivyo Alivyoichinja KMC

HUYU Luis Miquissone ameshindikana! Ndivyo unaweza kusema baada ya raia huyu wa Msumbiji, jana kufunga mabao mawili ya haraka haraka na kuiongoza Simba kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Hilo na bao la tatu kwa Luis tangu atue hivi karibuni kuichezea Simba na ametoa salamu kuelekea mchezo dhidi ya Yanga Jumapili hii. Alifunga bao la kwanza kwa shuti la ndani ya eneo la hatari dakika ya 70, akitumia vizuri pasi ya mwisho ya Clatous Chama.

 

Bao la pili alifunga dakika ya 71 baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa KMC, kufuatia Deo Kanda kupiga shuti likaokolewa ndipo lilipomkuta Luis aliyetumbukiza mpira kimiani.

 

Simba walishambulia kipindi cha kwanza lakini hawakupata bao na ilionekana kama mechi hiyo inakwenda kuisha kwa sare. Mara baada ya Luis kufunga mabao hayo, alitolewa katika kile kinachoonekana ni kumpumzisha ili awasubiri Yanga. Nafasi yake ilichukuliwa na Sharaf Shiboub.

 

Dakika ya 12, Simba waliingia katika boksi la KMC, Bocco akapiga shuti ambalo lilipanguliwa na kipa. Dakika ya 22, Shomary Kapombe alipiga krosi ambayo iliguswa na Clatous Chama lakini mpira ukatoka nje kidogo ya lango.

 

Dakika moja baadaye, Charles Ilamfya naye aliingia kwenye boksi la Simba na akapiga shuti kali lililopanguliwa na Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa bao. Dakika ya 24, Luis Miquissone alipiga kichwa safi akiunganisha krosi ya Kapombe lakini mpira uligonga mwamba.

 

Dakika ya 42, Ilamfya alionekana kumpiga kiwiko beki wa Simba, Pascal Wawa lakini mwamuzi aliamua kuwa hakuna chochote kibaya kilichofanyika. Dakika mbili baadaye, Luis alipiga shuti lililogonga mkono wa Ismail Gambo ndani ya boksi lakini mwamuzi anaamua mpira uendelee.

 

Timu zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana. Lakini kipindi cha pili, Simba walianza kwa kasi na kufanya mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa bao. Sasa Simba wamefikisha pointi 65 wakionekana hawakamatiki. Azam inafuatia ikiwa na pointi 48, Namungo ina 46 na Yanga ina 44.

 

Simba: Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/Deo Kanda dk 63, Clatous Chama/Ibrahim Ajibu dk 81, John Bocco, Luis Miquissone/ Shibob dk 75 na Francis Kahata.

 

KMC: Jonathan Nahimana, Kelvin Sospeter, Ally Ramadhan, Ismail Gumbo, Sadala Mohamed, Kenny Ally, Hassan Kabuda, Emmanuel Mvuyekule, Charles Ilamfya/Salim Aiyee dk 65, Hassan Kaparata/ Mohamed Samatta dk 85 na Sergy Alain/James Msuva dk 76.

Said Ally | Dar es Salaam

Leave a Comment