Luxembourg imekuwa nchi ya kwanza duniani kufanya usafiri wa umma kuwa wa bure (mwananchi hatolipa nauli). Lengo ni kuondoa msongamano wa magari katika maeneo ya katikati ya miji.
Usafiri utakuwa bure kutoka Jumamosi, hatua ambayo itahusu asilimia 40 ya familia nchini humo na kuokoa kiasi cha Euro 100 kwa kila mtu kwa mwaka.
Magari binafsi yanahusika zaidi katika usafiri nchini humo ambapo utafiti wa mwaka 2018 ulionyesha kwamba magari madogo huchukua asilimia 47 ya usafiri wa kibiashara na asilimia 71 kwa safari za burudani. Mabasi hufanyiza asilimia 32 kwa watu kwenda kazini ambapo treni ni asilimia 19.
Jiji la Luxembourg ambalo limekuwa likijenga mfumo maalum wa treni za umeme bado linakabiliwa na msongamano mkubwa wa magari licha ya mfumo huo kuanza kutumika mwaka 2017. Pamoja na hayo, bado ujenzi unaendelea kuunganisha viunga vya kusini mwa jiji hilo na vya kaskazini ambako kuna uwanja wa ndege.
