DITRAM Nchimbi, mshambuliaji wa Yanga amesema kuwa ikitokea amepata nafasi atahakikisha anaitungua Simba.
Nchimbi, Jumamosi iliyopita alifunga mabao yote mawili ya Yanga waliposhinda 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu Bara na kusaidia kuipa pointi tatu muhimu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Nchimbi mwenye mabao matano na asisti mbili ndani ya ligi, alisema akipata nafasi kwenye mchezo wowote ukiwemo unaosubiriwa kwa hamu dhidi ya Simba, atahakikisha anafunga na kuisaidia timu yake kufanya vizuri.
“Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira, ikitokea mwalimu akinipanga kucheza kwenye mchezo wa Simba, nitapambana kuipa timu matokeo.
“Mwalimu amekuwa akituelekeza mambo mengi ya kufanya nasi tunayafanyia kazi, ila mambo bado kwani tuna mechi nyingi na ngumu ikiwa ni pamoja na mechi yetu dhidi ya Simba.
“Kwa sasa akili zetu ni kwenye mechi zetu za mbele, tunahitaji kupata pointi tatu na hilo linawezekana kwa kuwa tunashirikiana,” alisema Nchimbi.
LUNYAMADZO MLYUKA, Dar es Salaam