WAKATI dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) – ARVs, pamoja na dawa za kutibu mafua, zikidaiwa kutumika kutibu walioambukizwa virusi vya Corona, imebainika kuwa damu ya watu waliopona ugonjwa huo pia, inatibu wagonjwa wapya wa Corona.
Hatua hiyo imekuja wakati taarifa za hadi kufikia Februari 29 mwaka huu, zikionesha watu 85,688 duniani wameambukizwa Corona, vifo 2,933 vimeripotiwa kutokea katika maeneo mbalimbali huku watu 39,764 wakiripotiwa kupona ugonjwa huo hatari.
Kutokana na janga hilo ambalo lilianzia katika mji wa Wuhan nchini China, Gazeti la New York Times limeripoti kuwa maofisa wa afya nchini China, wametoa wito kwa watu waliopona ugonjwa huo kujitokeza kujitolea damu.
Kwa mujibu wa kampuni ya China National Biotec Group, imeeleza kuwa seli za damu ya mtu mmoja aliyepona ugonjwa huo, zinaweza kutibu watu 10 wenye Corona na kupunguza makali ya ugonjwa huo ndani ya muda wa saa 12 hadi 24.
Profesa wa baiolojia na sayansi ya mifumo ya fahamu kutoka Chuo kikuu cha New York, Carol Shoshkes Reiss alisema kuwa seli zilizopo kwenye damu ya mtu aliyepona ugonjwa huo, zina kinga ya kutosha kutibu mgonjwa mwingine kwa haraka zaidi.
“Ninafuraha kuona tunapiga hatua katika tafiti hizi za kisayansi kutibu ugonjwa huo, kwa sababu kitendo cha kumuwekea mgonjwa wa Corona seli za aliyepona Corona, ni hatua kubwa ambayo sasa inabidi kufanya tafiti zaidi za kisayansi ili kupata suluhu ya kutosha kuhusu ugonjwa huu,” alisema.
ARVs ILIPOTIBU CORONA
Ikumbukwe kuwa Februari 15 mwaka huu, Mwanafunzi raia wa Cameroon alisimulia jinsi dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi zilivyomponya Corona (covid-19).
Aidha, mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 21 aliyeambukizwa virusi hivyo nchini China, alisema katika kipindi chote cha matibabu yake yaliyodumu kwa siku 13, alikuwa akipewa dawa za antibiotiki na za ARV.
Kem Senou Pavel Daryl anayeishi katika mji wa Guangzhou alisema alianza kupata homa kali, kukohoa vibaya na kuonyesha dalili za mafua na baada ya vipimo, aligundulika kuambukizwa virusi vya corona.
Akisimulia mkasa huo, mwanafunzi huyo alisema ingawa alikuwa katika maumivu makali, hakuwa na mpango wa kuondoka China hata kama hilo lingewezekana.
“Niliwaza sana, chochote kitakachofanyika sitaki kupeleka ugonjwa Afrika,” alisema mwanafunzi huyo akiwa katika chumba eneo maalumu alilotengwa kwa siku 14 sasa.
Alisema alipokuwa akienda hospitalini kwa mara ya kwanza, aliona kifo lakini baada ya kupewa dawa za kutibu wagonjwa walio na virusi vya ukimwi na antibiotic kwa wiki mbili, alianza kuonesha dalili ya kupona.
Pavel Daryl ni mtu wa kwanza mwenye asili ya Afrika aliyepona baada ya kuambukizwa virusi hatari vya corona ambako sasa umeingia barani Afrika. Misri ni nchi ya kwanza kuthibitisha kisa cha maambukizi ya virusi vya corona.
STORI: GABRIEL MUSHI, DAR
