RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ameinyooshea kidole cha lawama Somalia akisema hatua ya wanajeshi wa Somalia kuingia Kenya ni kitendo cha uchokozi, na kusema kwamba “Kenya haitaendelea kuvumilia hali hiyo.”
Jumatano wiki hii Kenyatta aliitisha kikao cha dharura cha baraza lake la usalama la kitaifa siku mbili baada ya mapiganoyaliyotokea Jumatatu Machi 2, 2020, kati ya jeshi la Somalia na lile la jimbo linalojitawa la Jubaland ambapo mapigano hayo yalitokea karibu na mpaka na Kenya.
Serikali ya Kenya imeishutumu serikali ya Mogadishu kwa kukiuka sheria ya uhuru wake na kuingia nchini humo.
Kwa mujibu wa Kenya, mapigano kati ya wanajeshi wa Somalia na wale wa Jubaland yalisababisha askari wa Somalia kuingia katika mji wa mpaka wa Kenya wa Mandera, ambapo “waliharibu mali za raia” na waliwatishia usalama wakazi wa mji huo.”
Kenya imesema katika taarifa, ikieleza kwamba “kitendo hicho cha uchokozi” haitaendelea kukifumbia macho.
Wabunge kutoka mji wa Mandera waliliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu kwamba mashambulizi hayo yalikuwa mabay,a hali iliyowafanya wakazi kuyatoroka makazi yao wakihofia usalama wao.
”Acheni uchokozi wa mara kwa mara na badala yake angazieni mambo yenu ya ndani”, amesema Kenyatta, akiongeza kwamba “Kenya haitakubali kutumika kama sababu ya changamoto zinazoikumba Somalia kisiasa.
“Kenya imelazimika kuathirika pakubwa kutokana na hatua yake ya kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuweka amani na usalama katika nchi jirani ya Somalia,” ameongeza kiongozi huyo wa Kenya.
Mapigano hayo ya Somalia hivi karibuni yanatokana na wasiwasi kati ya serikali ya Mogadishu na serikali zake za kijimbo.
Mamlaka ya Jubaland mnamo mwezi Agosti iliishutumu Mogadishu kwa kuingilia uchaguzi wake na kutaka kumpindua rais wa jimbo hilo, Ahmed Madobe, ili kupata uwezo wa kulidhibiti jimbo hilo.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne asubuhi wiki hii, Umoja wa Mataifa ulisema watu 56,000 walilazimika kuyatoroka makazi yao nchini Somalia kwa sababu ya mvutano katika Jimbo linalojitawala la Jubaland.
