LEO Jumapili kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi, Namungo FC itaikaribisha Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa Namungo kumenyana na Yanga tangu ilipopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu huu. Namungo hadi sasa imecheza mechi 27 na kujikusanyia pointi 49 ikiwa nafasi ya nne huku Yanga ikiwa imecheza mechi 26, imevuna pointi 50 ikiwa nafasi ya tatu.
Namungo ni hatari kwa kushambulia ambapo kwenye mechi zao 27 sawa na dakika 2430, wamefunga mabao 33, Yanga kwenye mechi 26 sawa na dakika 2340, wamefunga mabao 30.
Ubovu wa Namungo ni kwenye ulinzi ambapo wamekubali kufungwa mabao 24, huku Yanga ikifungwa mabao 19.
Ni wazi pointi tatu za mchezo wa leo ni za moto kwani kila upande unazihitaji kwa nia ya kujiweka kwenye
nafasi nzuri. Namungo ikishinda, inaishusha Yanga, na Yanga ikishinda basi itaikimbia zaidi Namungo.
Kocha wa Namungo, Hitimana Thiery, amesema: “Yanga wawe tayari kwa kupokea maumivu mengine, kwa sababu hatuna namna ya kuwaacha washinde katika mchezo huu, tuna historia nzuri tukiwa nyumbani, lakini mbali na hilo mechi hiyo, itaamua nani atakaa nafasi ya tatu.
“Nimezungumza na vijana wangu, tumekubaliana namna ya kucheza na Yanga kwa kuwa tumetizama video za michezo yao ili kujua namna gani wanacheza, hivyo tumeshafanya maandalizi kulingana na ubora wa timu hiyo na bila shaka tutashinda.”
Upande wa Yanga, Kocha Mkuu, Luc Eymael, amesema: “Hii ni mechi ngumu kwetu kwa sababu kwanza tunacheza sehemu siyo nzuri lakini wapinzani wetu wana timu nzuri.
“Ni vita ya nafasi ya tatu na nne, tunatakiwa kucheza kwa juhudi kubwa.
“Namungo ni timu ambayo imetoka daraja la kwanza, lakini inafanya vizuri hivi sasa, tunatakiwa kupambana kupata pointi kwao. Uzuri
ni kuwa tunaenda tukiwa na wachezaji wote akiwemo Morrison (Bernard) ambaye mechi iliyopita hakuwepo.”
