×

Mjengo Mpya wa Lyyn Waibua Maswali

 

KAMA ulikuwa hujui, habari ikufikie kwamba, mrembo Lyyn amehamia kwenye mjengo mwingine wa maana huko Masaki jijini Dar. Lakini mbali na kuhamia kwenye mjengo huo mpya, maswali yameibuka kuhusu mjengo huo mpya.

 

CHANZO KILIANZA KUPENYEZA

Awali, chanzo makini kilipenyeza ubuyu kuwa, mrembo huyo ambaye anaishi maisha yenye hadhi kubwa, amehama kwenye mjengo wa kifahari aliokuwa anaishi maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar.

“Nahisi itakuwa ni kushindwa masuala ya kodi, si unajua tena mastaa hawa mambo yao, analazimisha kuishi maisha ya juu halafu ndani ya muda fulani mambo yakimshinda, anarejesha majeshi.

 

AMEHAMIA MASAKI

“Nimesikia kwa sasa amehamia Masaki, mnaweza kufuatilia ili kujiridhisha kama ameshuka hadhi au amepanda, lakini kimsingi inaonesha ameshindwa kodi ya Mbezi,” kilisema chanzo makini.

AMANI LASAKA UKWELI

Katika kusaka ukweli wa mambo, ndipo Amani lilipokutana na maswali yanayohusu mjengo huo mpya.

Amani lilianza kwa kutinga kwenye nyumba ya Mbezi aliyokuwa anaishi mrembo huyo na kujiridhisha kuwa amehama na jirani mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake, aliweka wazi kuwa Lyyn amesepa.

“Hayupo hapa, ana kama wiki kadhaa sasa lakini hata huko Masaki alikohamia mimi napajua, naweza nikawaelekeza,” alisema jirani huyo.

 

MASWALI YAIBUKA

Baadhi ya majirani waliozungumza na Amani ambao wanamjua kiundani mrembo huyo, ndio waliibua maswali ambayo kimsingi yanafikirisha kuhusu jengo hilo jipya.

Walihoji anapata wapi hiyo jeuri ya kuhamia kwenye nyumba ya ghorofa, tena wakati huu ambao watu wengi wanalia hawana kitu?

 

Wengine walienda mbali kwa kusema, kazi ya muziki anayoifanya inamuingizia kiasi gani wakati bado hajaonekana akifanya shoo yoyote kubwa na kujaza watu akiwa peke yake.

Lakini wengine walisema kama kuna mwanaume aliye nyuma yake, mbona hawajawahi kumuona akiishi naye zaidi ya kuonekana na mabinti wake anaoishi nao?

 

Kama hiyo haitoshi, wengine walisema hata kama ana biashara inayomuingizia fedha nje ya muziki, mbona hawajawahi kuona anaitangaza au anaifanya?

Ukiachana na hilo, wengine waliachana tu na ghorofa hilo jipya lakini walienda mbali kwa kuangazia nyumba zote za gharama alizowahi kuishi ikiwemo ile ya Goba.

“Hebu angalia, yeye anabadili tu maghorofa tena kodi zake sio za mchezo mchezo, anapata wapi hii hela?” Alihoji mmoja wa majirani hao na kuongeza:

“Hata yale magari ya kifahari anayoendesha, kwa kweli tunashindwa kuelewa anayamiliki kwa kipato gani anachoingiza.”

 

HUYU HAPA MWENYEWE

Akijibu maswali hayo yaliyoibuliwa kuhusu nyumba hiyo mpya, Lyyn alianza kwa kuwashangaa wanaofikiri amefulia na kahamia nyumba yenye hadhi ya chini.

Alisema kuwa yeye si mtu wa kushuka kama wanavyodai, ila amehama ili kubadilisha mazingira.

 

“Kuhusu mimi kuhama kwenye ile nyumba eti nimefulia kama watu wanavyosema, siyo kweli. Nimehama kwa kuwa nimepata nyumba nzuri zaidi ya ile, nyumba yenyewe kwanza ipo Masaki, sasa hapo kwa kawaida nimeshindwa au maana kule nilikuwa nalipa milioni moja na laki tano lakini Masaki nalipa milioni 3, wanaweza wakapiga hesabu wao wenyewe,” alisema Lyyn.

 

Kuonesha kwamba anachokizungumza anamaanisha, mrembo huyo alimtumia mwanahabari wetu video inayoonesha mandhari ya mjengo huo.

 

 

TUJIKUMBUSHE

Mrembo huyo amekuwa akiishi maisha ya thamani ya juu, lakini kumekuwa na usiri mkubwa juu ya nani au nini kinachompa jeuri hiyo.

Kabla ya kupanga nyumba hiyo ya Masaki, alipanga nyumba ya kifahari Goba kisha akahamia kwenye bangaruu hilo la Mbezi Beach.

Stori: Neema Adrian, Amani

Leave a Comment