KOCHA Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, jana Jumatano alitarajiwa kukutana na uongozi wa timu hiyo kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wachezaji akiwemo David Molinga juu ya suala la matukio ya utovu wa nidhamu.
Mbelgiji huyo wiki iliyopita alitoa malalamiko kwa uongozi akiwatuhumu baadhi ya wachezaji ambao hawakusafiri na timu kwenda Ruangwa mkoani Lindi kucheza dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Majaliwa na kumalizika kwa sare bao 1-1.
Kati ya wachezaji wanaotajwa kugomea safari hiyo ni Mkongomani, David Molinga ambaye inaelezwa aligoma baada ya mashabiki kumzomea mara baada ya mchezo dhidi ya KMC uliopigwa Uwanja Uhuru, Dar kutokana na kukosa nafasi kadhaa za kufunga mabao.
Katika mechi hiyo, Yanga ilifungwa 1-0. Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amethibitisha kuwepo kwa kikao hicho ambacho maamuzi yake yanaweza kuwaweka matatani baadhi ya nyota.
“Tumemsikia kocha akitoa malalamiko yake kuhusu baadhi ya wachezaji lakini jana (juzi) alikutana na uongozi na kukaa nao pamoja kujadili masuala hayo kwa kina. “Katika hilo, mwisho wa siku yeye mwenyewe ndiye atakayekuwa na maamuzi ya mwisho kuhusu hatua ambazo zitapaswa kuchukuliwa,” alisema Bumbuli.
WILBERT MOLANDI, DAR

