×

Corona Yawatesa Mastaa

DAR: Siku chache baada ya kuripotiwa kuwepo kwa wagonjwa kadhaa wenye Virusi vya Mafua ya Corona (COVIC-19) nchini, kwa namna moja au nyingine, ugonjwa huo umewaathiri mastaa wengi wa Kibongo, IJUMAA limekukusanyia data za kutosha.

 

Taarifa ambazo IJUMAA limezipata ni kuwa, mastaa ambao walikuwa wakifanya biashara mbalimbali nje ya Bongo hususan China, Marekani na Ulaya, wapo kwenye msoto mkali kufuatia msimamo wa nchi hizo katika kudhibiti ugonjwa huo ulioenea kwa kasi katika nchi nyingi duniani.

 

KUSOTA…

Mastaa ambao wapo kwenye msoto ambao IJUMAA limewanasa kwenye uchunguzi wake ni Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Faiza Ally, Shamsa Ford, Salma Jabu ‘Nisha’, Jacqueline Wolper na Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ na wengine wengi waliokuwa na madili tofautitofauti nje ya nchi.

 

IJUMAA limezungumza na mtu aliye karibu na mastaa ambaye ameweka wazi kuwa mastaa hao wapo kwenye wakati mgumu kwani walikuwa na harakati za kufanya kwenye nchi tofautitofauti, lakini Corona imewaharibia ‘ramani’.

 

“Kuna ambao walikuwa wanakwenda kufanya biashara kama China, mtu kama Shamsa, Faiza na Wolper walikuwa wanakwenda China kwenda kuchukua bidhaa na kuuza Bongo, sasa kule sasa hivi Serikali imeweka utaratibu wa kuwaweka kwenye uangalizi maalum wa siku kumi na nne kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao.

 

“Sasa hiyo imewaathiri sana. Wao walikuwa wakienda kule hawakai siku nyingi ili kuepuka gharama, kwa sasa ukienda unalazimika kukaa siku nyingi zaidi ili uweze kuangaliwa kama una maambukizi au la,” alisema mtu huyo aliye karibu na mastaa.

 

IJUMAA lilizungumza na mwigizaji Nisha ambaye alikiri kuathiriwa na tatizo la Corona katika biashara zake.

“Corona imetuathiri sana. Huwezi kwenda China ukaweza kuwa na bajeti ya kukaa kule karibu mwezi mzima,” alisema Nisha.

 

SHOO ZASIMAMA

Kwa upande mwingine, mtu huyo aliwazungumzia pia wasanii ambao walikuwa wanakwenda kufanya ziara za kimuziki akiwemo Diamond au Mondi na Nandy.

“Hawa wote ni ngumu kwa sasa kwenda katika zile shoo zao maana kama ulivyosikia, Rais Magufuli (Dk John Pombe) ameshasema kwamba hakuna kusafiri hovyo.

 

“Sasa kwa kuwa Serikali ndiyo inayotoa kibali, si rahisi kwa sasa wakatoa kibali cha mtu kutoka nje ya nchi maana ni kujiweka kwenye hatari ya kuleta maambukizi pindi atakaporejea nchini,” alisema mtu huyo na kuongeza;

“Hii ni mpaka pale hali itakapokuwa shwari, hivyo itategemea. Wanaweza wakakaa muda mrefu zaidi au pia yawezekana ikawa ni ndani ya muda mfupi.”

 

RATIBA ZAO

IJUMAA linafahamu, ratiba ya Nandy Marekani inaonesha atapafomu Mei 22, mwaka huu katika Mji wa Columbus, Mei 23 (Houston), Mei 24 (Iowa), Mei 29 (New York) na Mei 30 ni Boston.

Kisha, mrembo huyo anayetamba kwa sasa na Wimbo wa Na Nusu, Juni 5 alitarajia kufanya shoo Atlanta, Juni 6 (Chicago), Juni 12 (Los Angeles), Juni 13 (Seattle), Juni 19 (Denver), Juni 20 (Minnesota), Juni 26 (North Carolina na kumalizia Washington DC Juni 27.

 

KWA UPANDE WA MONDI…

Mondi ratiba yake ilikuwa afanye shoo Marseille, Ufaransa (Aprili 3), Stockholm Sweden (Aprili 4), Abidjan na Ivory Coast (Aprili 18).

 

Kisha Antananarivo, Madagascar (Juni 1), Reunion Island (Juni 6), Majunga, Madagascar (Juni 7), Ambanja, Madagascar (Juni 12), Antalaha, Madagascar (Juni 14), Comores Island (Juni 19), Mayotte Island (Juni 20) na hatimaye atamalizia Amsterdam nchini Uholanzi (Julai 4).

 

Hivyo kutofanyika kwa shoo hizo, kutawasababishia mastaa hao kukosa mapato huku wale wa biashara, wakikosa bidhaa na kushindwa kufanya biashara.

 

WENGINE WANENA

Kutokana na janga hilo, baadhi ya mastaa wamenena juu ya hofu waliyonayo;

 

CHUCHU HANS

Kwa upande wake mwigizaji wa filamu za Kibongo, Chuchu Hans amesema;

“Ni kitu ambacho kinatisha sana na kinakosesha amani, cha msingi ni kuomba kwa sababu tumejisahau sana na kumekuwa na matukio ya kutisha, inaweza ikawa ni kwa sababu Mwenyezi Mungu amechukia hivyo anatukumbusha kumrudia yeye. Pia tufuate maelekezo ambayo Serikali inatoa ili kujikinga na janga hili la Corona.”

 

BILLNASS

Mwanamuziki wa Bongo Fleva, William Lymo ‘Billnass’ naye kwa upande wake amefunguka kuhusiana na janga hili; “Kwa upande wangu nina hofu sana na hivyo virusi na nimekuwa nikifuatilia kwenye vyombo vya habari ili kuendelea kupata taarifa ya kile kinachoendelea na ninamuomba sana Mwenyezi Mungu kwa sababu Corona haina kinga wala tiba na hili si suala dogo. Ninawashauri Watanzania wenzangu tufuate maelekezo.”

 

KHADIJA KOPA

Naye malkia wa Mipasho kwenye muziki wa Taarab, Khadija Kopa, ametoa ya kwake juu ya Corona kwa kusema kuwa wasanii watumike kutoa elimu kwa jamii;

 

“Naona hili jambo ni kubwa na watu wamekuwa wakifanya mzaha, hili jambo si la kuchezea, ni bora kufuata ushauri kwa kukaa nyumbani maana hata sisi wasanii, kazi zetu tumeacha ili kutulia kwanza na kuangalia hali inaendaje. Kwa wasanii tujitahidi kutoa elimu kwa jamii kwa njia yoyote ili kujikinga na haya maambukizi ya Corona maana sisi ni kioo cha jamii.”

 

LULU DIVA

Mwanadada anayefanya Bongo Fleva, Lulu Abass ‘Lulu Diva’ kwa upande amesema kuwa anaogopa mno;

“Yaani mimi naogopa sana huu ugonjwa tangu nimeusikia na ukizingatia mimi ni mzembe sana, huwa ninachukulia mambo kawaida tu, kikubwa tujilinde.”

 

Kwa upande wake mkongwe kwenye Bongo Fleva, Hamis Mwinjuma ‘Mwana-FA’ alifunguka; “Tahadhari ni muhimu sana kwenye hili la Corona. Ila kupaniki ndiyo hakufai. Kama ulikuwa hujui, paniki yenyewe inapunguza kinga ya mwili. True story. Tukichukua tahadhari, tukafuata maelekezo yanayotolewa na wataalam (sio redio mbao hizi) namna ya kujikinga na hata kujitibu na kujiangalia iwapo utatufikia, tutakuwa sawa tu.

 

0800110124 na 0800110125 ndizo namba za bure za kupiga kama utaona una dalili au kuna mtu ana dalili za Corona.”

Kwa upande wake msanii wa mduara, Zuwena Mohammed ‘Shishi’ amesema; “Tuchukue tahadhari, Mungu atatulinda, inshaallah!”

Stori: MWANDISHI WETU, Ijumaa

Leave a Comment